Kikao cha Bunge Maalum la Katiba. |
Kama mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba
utaendelea kama linavyokwenda, uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, unaweza kusogezwa mbele
hadi mwakani.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo jana alipozungumza na
waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Pinda alisema muda uliopangwa kwa ajili ya Bunge Maalumu ni siku 70,
lakini mpaka sasa kazi iliyofanyika ni moja, ya kutengeneza kanuni, na
tayari siku 38 mpaka jana zimeisha, bado kazi rasmi ya kujadili rasimu
haijaanza.
"Hatari ya kusogeza mbele uchaguzi wa serikali za mitaa ninaiona
dhahiri, nadhani itabidi tu tumuombe Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete,
tusogeze mbele uchaguzi huu, ili kutoa nafasi kwa kazi zingine kuendelea
hususan ya kutengeneza Katiba," alisema Pinda.
Mbali na uchaguzi huo, Pinda pia anapanga kupendekeza bunge hilo
lisitishwe, ili kupisha muda wa Bunge la Bajeti kuanza kisha la Katiba
liitishwe tena.
Alisema kama kazi ya bunge hilo itakuwa haijamalizika ifikapo
mwishoni mwa Aprili mwaka huu, hatakuwa na namna isipokuwa kumuomba Rais
Kikwete aliahirishe ili lipishe Bunge la Bajeti liendelee na kazi zake.
"Hatuwezi kuacha kazi zingine za serikali zikasimama, lazima
ziendelee, na zitaendelea kama bajeti za wizara zitapitishwa, nadhani
kama hatutakwenda sawa, tutamuomba tu Rais aahirishe bunge hili la
Katiba, tufanye kazi hii nyingine iliyo mbele yetu.
"Tulijipangia siku 70, lakini tukasema kama hatutakuwa
tumeikamilisha, basi tuongeze zingine 20, lakini kwa mwendo huu uliopo,
sidhani kama tutaimaliza, nadhani inahitaji muda zaidi," alisema Pinda.
Wakati huohuoWaziri Mkuu Pinda alionya wajumbe wa bunge hilo kuacha
kuwapotosha wananchi kuhusu hotuba zilizotolewa bungeni na Rais Kikwete
na Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba.
Alisema baadhi wanataka kuuaminisha umma kuwa rasimu iliyowasilishwa
bungeni na Jaji Warioba ikishajadiliwa na wajumbe ndiyo mwisho inapaswa
kupitishwa.
"Umma ningependa ufahamu kuwa rasimu ile si mwisho wa kila kitu, bado
inapaswa kujadiliwa na kuboreshwa na watu wa makundi mbalimbali,"
alisema Pinda.
Alisema hata Rais mambo aliyoyazungumza katika hotuba yake, yanalenga
kuboresha na pia ni hoja zake ambazo wajumbe na Watanzania wanapaswa
kuzijadili, kwa kuwa yeye pia ni miongoni mwa wananchi mwenye uhuru wa
kutoa maoni.
"Na ndiyo maana katika kila alipokuwa akishauri jambo ama kutoa maoni
yake kuhusu vifungu vilivyomo ndani ya rasimu, mwisho alisema haya ni
maoni yangu, mnaweza kuyajadili ama kuyaacha," alisema Pinda.
Alisema kitendo cha baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa siasa ndani
ya bunge hilo kutaka kuuaminisha umma kuwa Rais Kikwete aliwasilisha
maoni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanalenga kupotosha ukweli.
"Ni kweli Rais ni Mwenyekiti wa CCM, ni dhahiri anaweza kubeba hisia
za kichama, hilo lipo wazi, hata kama leo Profesa Lipumba ama Mbowe
wangekuwa ni marais, na wenyeviti wa vyama vyao, hawataweza kuacha
kubeba hisia za vyama vyao, huo ndiyo ukweli," alisema Pinda.
Alisema Rais alifanya kazi yake kama kiongozi wa nchi mwenye
kupongeza pale palipo na mafanikio na kukosoa penye upungufu na kushauri
kipi kifanyike.
"Binafsi sioni kama kuna mahali Rais Kikwete alikosea, bali maneno
haya yanayoendelea dhidi ya hotuba ile yana lengo la kupindisha ukweli,"
alisema Pinda.
Akizungumzia kero tatu za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi,
alisema ni vyema wajumbe wakazijadili kwa kina ili katiba itakayoundwa
ije na majibu.
Kero hizo ni pamoja na ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri, ardhi na utambulisho wa kitaifa.
Aliasa wajumbe wasikubali kupoteza utambulisho wa watu wa Zanzibar kwa makusudi.
No comments:
Post a Comment