Gari ya magereza itumikayo kubeba wafungwa na mahabusu.
Askari
Polisi watano na wafanyabiashara saba wamefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kinondoni Jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na kesi tatu
tofauti ikiwamo unyang’anyi wa kutumia bastola na panga na kufanikisha
uporaji wa mali zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 100.
Katika kesi ya kwanza, Meneja wa Kituo
cha Mafuta cha GBP, Germano Chaba (30), mfanyabiashara Salum Musa (22),
Koplo Rajabu Ugolo (39), Konstebo Albanus Kosa (32), mfanyabiashara
Bahati Ahmed (35), Konstebo Salimon (30) na Kostebo Seleman (36)
wanadaiwa kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia bastola na panga.
Washtakiwa hao walisomewa mashtakiwa yao mbele ya Hakimu Mkazi Athuman Nyamlani.
Wakili wa Serikali, Mmassy Bondo alidai
kuwa, Februari 17, mwaka huu eneo la Boko Basihaya, katika kituo cha
mafuta cha GBP, jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliiba Sh. 77,379,240
mali ya kampuni hiyo.
Washtakiwa walikana mashitaka hayo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na
washtakiwa watasomewa maelezo ya awali Machi 28, mwaka huu.
Katika kesi ya pili, Rajabu Mkendwa,
Juma Ngwele, Konstebo Albanus, Musa, Omary Juma, Charles Mbelwa, Adamu
Mkombozi, Ally Salum na Gerad Matutu walisomewa shitaka la unyang’anyi
wa vitu mbalimbali vya ndani vyenye thamani ya Sh. milioni 4.5, mali ya
Hong Tang.Ilidaiwa kuwa mara na kabla ya tukio hilo washtakiwa
walimtishia kwa bastola na panga Suzan Juan na Nelson William.
Washtakiwa walikana mashitaka yao mbele
ya Hakimu Mkazi Benedicta Beda na Wakili wa Serikali Hilda Kato alidai
kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.Hakimu Beda alisema kesi
hiyo itatajwa Aprili 3, mwaka huu.
Katika kesi ya tatu, washtakiwa Musa,
Omary Hamis, Mkombozi na Mbelwa walisomewa shitaka la unyang’anyi wa
kutumia silaha mbele ya Hakimu Mkazi Selemani Mzava.
Wakili wa Serikali Tumaini Mfikwa alidai
kuwa, Machi 6, mwaka huu maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam,
washtakiwa waliiba vitu mbalimbali vikiwa na thamani ya Sh. milioni 49
mali ya Deogratius Ngonyani.
Ilidaiwa kuwa mara na kabla ya
unyang’anyi huo, washtakiwa walimtishia kwa bastola Melisa Deogratias
ili kufanikisha uporaji huo.Kesi hiyo itatajwa Aprili 3, mwaka huu na
washtakiwa wote wamerudishwa mahabusu kwa kuwa mashtaka yanayowakabili
hayana dhamana
No comments:
Post a Comment