ASKARI
Polisi, Mohamed Mjomba (44) amepoteza maisha baada ya kushambuliwa na
majambazi, waliovamia Hoteli ya Kitalii ya Pongwe Uroa Wilaya ya Kati
Unguja.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Augostino Olommi alithibitisha kuuawa
kwa askari huyo. Aliongeza kuwa majambazi hao walivamia hoteli hiyo saa
nane za usiku kwa lengo la kufanya uporaji.
Olommi
alisema majambazi hao waliwateka na kuwaweka chini ya ulinzi walinzi wa
kawaida waliokuwepo hotelini hapo, lakini walipambana na upinzani kutoka
kwa askari Polisi, waliokuwa wakilinda hoteli hiyo kwa kurushiana
risasi, ambapo askari wawili walijeruhiwa.
Askari
aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi ya bega ni Ibrahim Juma (33), ambaye
amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja huku Mjomba akipoteza maisha
baada ya kujeruhiwa vibaya na majambazi hao, ambao hata hivyo
walikimbia.
“Jeshi la
Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwakamata wahusika
wote na kuwafikisha katika vyombo vya sheria,” alisema.
Olommi
aliwataka wamiliki wa hoteli na wafanyakazi, kutoa taarifa wakati
wanapotilia wasiwasi nyendo za watu wasiofahamika katika maeneo ya
hoteli za kitalii. Mjomba alizikwa jana kwa heshima zote za Jeshi la
Polisi kijijini kwao Bambi Wilaya ya Kati Unguja.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment