Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, March 17, 2014

NDOTO ZA BANDARI MPYA YA MBEGANI YAKAMILIKA

 Meneja Miradi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bw. Alexander Ndibalema (Kulia aliyesimama) akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, wawakilishi wa wanavijiji vya Mradi wa Bandari Mpya ya Mbegani na Timu ya Uthamini wa Ardhi wa eneo la mradi. Waliokaa viti vya mbele ni viongozi wa Timu ya ukaguzi, Bibi Florence Mwanri (Wapili Kulia) na Prof. Longinus Rutasitara (Watatu Kulia). Kushoto ni Mratibu wa ziara hiyo, Bibi Salome Kingdom.
 Mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kulia) akizungumza katika mkutano huo.
 Mthamini Mkuu wa Ardhi ya Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mrema (Kulia) akizungumza katika mkutano huo.
 Mwenyekiti wa Kijiji cha Pande, Bw. Ubezi Kondo (Kulia aliyesimama) akizungumza wakati Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipopita kijijini hapo kujua hali ya zoezi la tathmini ya ardhi kwa ajili ya mradi wa Bandari Mpya ya Mbegani. Kulia kwake ni Mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri na Mthamini Mkuu wa Ardhi ya Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mrema.
 Mwenyekiti wa Kijiji cha Pande, Bw. Ubezi Kondo (Kushoto) akionesha eneo itakapokuwepo Bandari Mpya ya Mbegani. Wanaotazama ni Meneja Miradi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bw. Alexander Ndibalema (Kulia), Mthamini Mkuu wa Ardhi ya Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mrema (Wapili Kulia) na Mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Watatu Kulia).
 Meneja Miradi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bw. Alexander Ndibalema (Kulia) akitoa maelezo juu ya maendeleo ya Mradi wa Bandari Mpya ya Mbegani katika eneo itakapokuwepo bandari hiyo. Wanaomsilikiliza ni Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. 
Picha na Saidi Mkabakuli

Na Saidi Mkabakuli
Ndoto ya kuwa na Bandari mpya ya Mbegani kufikia mwaka 2017 na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16) imekamilika kwa takribani asilimia 90 kufuatia kukamilika kwa tathmini ya ardhi ya eneo zima la mradi huo. 
Hayo yamedhihirishwa na Mthamini Mkuu wa Ardhi ya Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mrema wakati akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo.

Mhandisi Mrema alisema kuwa mpaka sasa jumla ya kaya 1100 kutoka vitongoji vya Bisibisi, Mji Mpya, Mlingotini na Pande vimeshafanyiwa tathmini, ambapo makadirio ya awali yanaonesha jumla ya shilingi bilioni 23 zinatarajiwa kulipwa kupisha mradi.
“Mpaka sasa takribani asilimia 90 ya eneo la mradi ambalo ni sawa na hekta 2000 limeshakamilika, ambapo kwa mujibu wa mapendekezo ya tathmini tunatarajia malipo kufanyika kufikia mwezi Juni mwaka huu,” alisema Mhandisi Mrema.
Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alisema kuwa kuna haja ya kuhakikisha fidia kwa wanavijiji hao inalipwa kwa wakati ili kuondoa usumbufu wa kusubiri malipo ya kwa muda mrefu hali itakayochochea kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi.
“Nawaomba muhakikishe malipo yanafanywa kwa wakati ili kuwaondoshea usumbufu wananchi ili kulinda heshima ya Serikali na kuondosha kero ya kusubiri ya kusubiri kwa muda mrefu,” alisema Bibi Mwanri ambaye ni Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia Huduma za Jamii na Maendeleo ya Idadi ya Watu.
Akijibu hoja ya ushirikishwaji wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Pande, Bw. Ubezi Kondo alisema kuwa kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakishirikishwa katika kila hatua ya uthamini huo. Aliongeza kuwa hali hii imewaongezea hamasa ya kuupisha mradi huo ili kutimiza ndoto ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete ya kujenga Bandari hiyo pamoja na ahadi aliyoitoa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1968.
“Kwa hakika tunaukubali mradi huu kwa mikono miwili ili kutimiza ndoto na ahadi za Rais Kikwete na ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1968 wakati akifungua Chuo cha Mbegani ambapo aliahidi kuwa atahakikisha kunajengwa Bandari ya kisasa Mbegani,” alisema Bw. Kondo.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara ambaye ni kiongozi mwenza wa ukaguzi huo, uwekezaji katika Bandari mpya ya Mbegani unatoa fursa za kimkakati katika kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16). 
“Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16) unaweka bayana kuwa uwekezaji wa Bandari ni mojawapo ya maeneo ya kipaumbele na kimkakati ambapo kukamilika kwa ujenzi wa bandari mpya ya Mbegani Bagamoyo kunatarajiwa kupunguza msongamano wa meli katika bandari ya Dar es Salaam,” alisema Prof. Rutasitara. 
Serikali imeaandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ukiwa na lengo la kuwa na mfumo madhubuti wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment