Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, March 5, 2014

Okwi, Kiiza watimka Yanga, uongozi wafanya maombi

Washambuliaji wa Yanga Hamis Kiiza 'Diego' na Emmanuel Okwi(kushoto).
Na Sweetbert Lukonge
WACHEZAJI wawili wa Yanga, Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi, wameondoka kwenye kikosi hicho na kujiunga na timu yao ya taifa.

Uganda inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Andora leo ambapo awali Yanga iliomba wachezaji wake hao wasijiunge na timu hiyo ili wajiandae kuivaa Al Ahly lakini shirikisho la Soka Uganda (Fufa) likagoma.
Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, ameliambia Championi Jumatano kuwa, wachezaji hao wanahitajika zaidi katika mechi ya marudiano ya Jumapili ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, hivyo kama wakikosekana itakuwa ni pigo kubwa kwao.
Alisema kutokana na hali hiyo ndiyo maana wameamua kuwaombea dua wasipatwe na majeraha yoyote watakapokuwa wanaitumikia nchi yao.
Hata hivyo, licha ya Fufa kutupilia mbali maombi ya Yanga juu ya wachezaji hao, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na lile la Rwanda (Ferwafa), yenyewe yamekubali maombi ya klabu hiyo na kuwaruhusu wachezaji wao kubaki kwenye kambi ya Wanajangwani hao.
“Tulijitahidi kadiri ya uwezo wetu wote kuhakikisha wachezaji hao hawajiungi na timu yao ya taifa, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya Fufa kukataa maombi yetu.
“Hata hivyo tunawaombea kwa Mungu waweze kuimaliza vizuri mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa bila ya majeraha yoyote yanayoweza kufanya washindwe kuitumikia klabu yao dhidi ya Al Ahly kwani mchango wao unahitajika sana,” alisema Njovu.
Okwi na Kiiza wameondoka nchini jana kwenda kujiunga na timu hiyo na watatakiwa kujiunga na wenzao nchini Misri keshokutwa.

Wachezaji hao watajiunga na kikosi cha Yanga nchini Misri tayari kwa kuitumikia klabu hiyo katika mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.chanzo Gpl

No comments:

Post a Comment