Dar es
Salaam. Wiki moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu kupangua wakurugenzi wizarani hupo, baadhi ya askari wa
wanyamapori wameibuka na kupinga uamuzi huo, huku wakitishia kufanya
mgomo.
Askari
hao zaidi ya 10 walioomba kutotajwa majina gazetini kwa usalama wa ajira
zao, wamepinga kuondolewa kwa Prof Alexander Songorwa kwenye nafasi ya
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori na badala yake kuteuliwa kwa Paul
Sarakikya kukaimu nafasi hiyo.
Mmoja wa
askari hao, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema kwa ujumla wao
wanashangazwa na jinsi Nyalandu alivyomwondoa kazini Prof Songorwa licha
ya kuwa alikuwa mtendaji mzuri aliyejali wafanyakazi na kuweka uzalendo
mbele.
"Profesa
Songorwa alikuwa Pori la Selous kufanya doria siku tatu kabla ya
kuondolewa kazini, alishirikiana na askari, hatua ambayo ni nadra sana
kufanywa na viongozi," alisema mmoja wa askari hao.
Alisema endapo Rais Jakaya Kikwete hatatengua uamuzi uliofanywa na Nyalandu, watafanya mgomo ambao utasababisha tembo kuuawa.
"Huyu mtu
amekaa wizarani kwa mwaka mmoja tu, amejitahidi kudhibiti matumizi
mabaya ya fedha, anajituma kiasi cha kulala porini, lakini leo
anaondolewa katika kazi bila sababu za kueleweka. Sisi tunahisi kuna
jambo hapa," alisema askari huyo huku akichagizwa na wenzake.
"Sisi tupo nyuma yake na hatutasita katika hilo. Kama anataka afukuze wizara nzima lakini siyo kumwondoa Songorwa."
Walisema
wana wasiwasi kuwa kuondolewa kwa Profesa Songorwa kumesababishwa na
utendaji wake mzuri hasa kudhibiti Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori
(TWPF) ambao pengine umesababisha baadhi ya watendaji ndani ya wizara
waliokosa masilahi kupeleka taarifa za uongo kumchongea Profesa
Songorwa.
Askari
hao walisema utendaji wa Profesa Songorwa ulikuwa wa pekee kwa aina yake
na aliweza kuendesha kitengo cha kiintelijensia kilichogundua baadhi ya
wafanyakazi wa maliasili kujihusisha na ujangili.
"Aliweza
kuwagundua wafanyakazi wa wizara ambao ni majangili na majina anayo kwa
nini asiachwe amalize kazi yake, badala yake anafukuzwa bila kosa."
Alisema mmoja wao.
Nyalandu akanusha:
Hata
hivyo, Nyalandu alikanusha tuhuma na lawama zilizorushwa kwake kuwa
amewapangua wakurugenzi kinyume na taratibu, akisisitiza kuwa alichukua
uamuzi huo kwa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment