Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, March 6, 2014

TAZAMA PICHA ZA VURUGU BUNGENI LEO NA TAARIFA KAMILI KUHUSU MZOZO ULIOTOKEA


Sehemu ya Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba wakitawanyika mara baada ya mwenyekiti kuahirisha kikao kutokana na baadhi ya wajumbe kutoelewana katika hoja.
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba,Mhe. Ole Sendeka akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tuhuma za baadhi ya wajumbe kuwa Mwenyekiti anampendelea kwa kumpa nafasi nyingi za kuchangia hoja katika semina ya kanuni za bunge maalum.
Mjumbe wa Bunge la Katiba na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo,Mhe. Freeman Mbowe akiongea na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo,mara baada ya kuahirishwa kwa kikao.
Mjumbe wa Bunge la Katiba,Mhe. Kajubi Mkajanga kutoka taasisi ya vyombo vya Habari akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mwemyekiti kulazimika kiuahirisha semina ya kujadili kanuni hadi saa kumi na moja (11:00) jioni.
Semina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba leo imelazimika kuahairishwa baada ya kuibuka vurugu ndani ya ukumbi wa Bunge. 
Zogo hilo liliumuka baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya wajumbe uliosababishwa na kutuhumiana kwamba zipo dalili za upendeleo wanazofanyiwa baadhi ya wajumbe kutokana na sababu za kiitikadi za vyama. 
Hali hiyo ya hewa ilichafuka  baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya Mjumbe Mhe. Christopher Ole Sendeka ambaye aliingia katika mvutano na Mjumbe wa Kamati ya Kanuni Mhe Abubakar Hamis Bakari kuhusiana na uwasilishwaji wa majedwali ya marekebisho ya kanuni. 
 Awali Mjumbe Sendeka alipewa ruksa na Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo Mhe Pandu Ameir Kificho,  awasilishe mapendekezo ya mabadiriko katika kifungu cha 58 cha kanuni hizo kilichokuwa kikijadiliwa muda huo. 
 Lakini baada ya Mhe Sendeka kuwasilisha mabadiriko yake, alisimama Mjumbe Bakari ambaye kiutaratibu alipaswa kujibu hoja hiyo hasa kwa kuwa ni mjumbe wa kamati ya kanuni. 
Mhe. Bakari alikataa kupokea hoja ya mabadiriko ya Mhe. Sendeka kwa kusema kuwa hayakuwa yamewasilishwa kwa kufuata taratibu za uwasilishwaji wa mabadiriko ya majedwali, na kwamba Kamati haina mapendekezo hayo hivyo haiwezi kujibu jambo lisilo jadiliwa. 
Katika kukataa huko Bakari alikitupia lawama kiti cha Mwenyekiti huyo kwa madai kuwa kimekuwa kikitaja majina ya wajumbe na kuwapa nafasi ya kuongea wakati hawapo kwenye utaratibu wala hawakuwa wameomba toka awali. 
 Aliongeza kuwa si kwa Mhe. Ole Sendeka pekee, bali pia Mwenyekiti huyo amekuwa akiataja wajumbe wengine wakiwamo Peter Serukamba pamoja na Umy Mwaimu ambao wote hawakuwa wamewasilisha majedwali ya mapendekezo ya marekebisho toka awali. 
 "Mheshimiwa Mwenyekiti, Ole Sendeka hayupo katika orodha ya walioleta mapendekezo, lakini nashangaa wewe unampa nafasi ya kuzungumza wakati hakuwapo kwenye orodha yetu, kamati hatuwezi kumpa nafasi ya kujibu hoja yake hatuitambui. 
"Hata hao wakina Ummy Mwalimu hawapo katika orodha. Mwenyekiti ukiendeleza huu mtindo wa kuruhusu kila anayetaka kuzungumza hapa azungumze hatutofika. tutatumia miezi 6 hapa kutengeza kanuni tu. Lazima uwe na maamuzi kuwa wanaoleta mapendekezo hivi sasa hatupokei"alisema Mhe Bakari 
 Baada ya Mhe Bakari kumaliza kuzungumza, Mhe Kificho aliingilia kati na kusema kuwa jambo hio linaweza kuwa limechanganywa na sekretarieti inayoandaa na kwamba yeye binafsi amepewa majina ya waliopeleka marekebisho hivyo anashangaa kuona kama hayapo kwa wajumbe hao. 
Mhe Kificho alitoa ruksa kwa Ole Sendeka kuongea tena, ambapo katika mazungumzo yake alitoa kaulia akisema kuwa mapendekezo yake aliyawasilisha mapema na kwamba kama Mhe Bakari ana itikadi zake za vyama asimuhusishe humo. 
 Mhe. Ole Sendeka alisema kuwa yeye ana uzoefu wa kanuni na kwamba alifuata taratibu akiwa na wenzakeMhe Serukamba pamoja na Mhe Mwalimu na kwama kama mapigo yao yanawaumiza wajumbe wengine wavumilie tu. 
 "Mheshimiwa mwenyekiti tuliopo hapa ni wajumbe. Nilijua na mimi sio dhaifu kwenye kanuni. Nnajua haki yangu kwa kuwasilisha kwa wakati, nilitimiza wajibu wangu, kama mapigo yetu yanawaumiza. 
 "Kazi yetu si kupeleka majina yetu kwa Abubakari, kama yeye ana chama chake na hoja zetu zinamuuma, asimame na kutuweka wazi kuwa yupo katika msimamo gani. Lakini mimi nimewasiisha kama taratibu zinavyonitaka"alisema Ole Sendeka 
 Kauli ya Mhe Sendeka ilianzisha sintofahamu ndani ya Bunge hilo baada ya baadhi ya wajumbe kuanza kuzomea na wengine wakisiama na kutaka kupewa ruksa ya kuzungumza huku wakiwasha vipaza sauti.
 Hali hiyo ilimuinua Mhe Kificho ambaye aliwasihi wajumbe kuacha kuingiza masuala ya vyama hasa kwakuwa wajumbe walioingia hapo ndani wamewakilisha makundi. 
"Niwaombe wajumbe tujitahidi sana, tusionyeshe misimamo ya vyama, tumepata heshima kubwa ya kuwapo humu ndani hivyo si vyema kuanza kuonesha vidole kwasababu huyu katika CCM, sijui CUF ama Chadema au kokote itaibua hisia ambazo si vyema.
 "Mheshimiwa Ole Sendeka naona ulimi umekwenda mbali kidogo ukamgusa mheshimiwa Bakari. Mimi naona hili jambo limekwenda nje. Kwa hiyo naomba tuwe makini"alisema Kificho Baada ya kauli ya Kificho, wajumbe walianza kupiga kelele wakitaka Mhe Ole Sendeka kumwomba radhi Mjumbe Bakari huku wengine wakimtaka asifanye hivyo. 
Mhe Kificho alitoa nafasi nyingine kwa Mhe Bakari kuzungumza, ambapo katika mazungumzo yake ndipo fujo hizo zilipoibuka. Katika Mazungumo yake, Mhe Bakari alisema kuwa alichosema yeye ni kwa faida ya Bunge na nchi, na kwamba taratibu ni kuwasilisha mapema mapendekezo na kwamba majina ya kina Sendeka hayakuwapo. 
 "Mimi nilizungumza vizuri hili kuweka utaratibu mzuri wa kupokea majedwali haya. Mheshimiwa mwenyeiti kwa bahati mbaya mdogo wangu Ole Sendeka anadai kanuni anazijua vizuri, lakini ninachosema sifikirii..sifikirii kama ana uzoefu wa kujua kanuni kunishinda mimi.
"Mheshimiwa mwenyekiti toka mwaka 1980 nipo katika mabunge haya, kwa hivyo sifikirii kama mtu katoka Simanjiro miaka kumi iliyopita anaweza akaja hapa na kusema anajua kanuni kunizidi. "Mimi sitaki aniombe radhi, ila ninachotaka kumfahamisha ni kwamba kuna watu wana ujuzi zaidi kuliko yeye hivyo awe makini katika mazungumzo yake"alisema Bakari 
Kauli hiyo ilizidisha mgawanyiko katika Bunge hilo, ambapo wajumbe walisimama na kuanza kupiga meza wengine wakizomea.  
Baadhi ya wajumbe walionekana wakirushiana maneno na hata kupeleka kutaka kurushiana makonde. 
 Hali hiyo ilipeleka askari ambao ni wapambe wa Bunge kusogea karibu ikiwa ni njia ya kutuliza vurugu hizo, huku wajumbe hao wakiendelea kurushiana maneno. 
 Vurugu hizo zilionekana kusambaa katika ukumbi mzima ambapo wajumbe wengine walionekana kurushiana maneno, hali iliyopelekea Mhe Kificho kuahirisha Semina hiyo.  NA MICHUZI BLOG

Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wakitoka Bungeni Mjini Dodoma Machi 6, 2014 baada ya Bunge hilo kusitihwa kwa muda kufuatia Sitofahamu iliyotokea. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd (wapili kushoto) wakijadili jambo na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kusitishwa kwa muda Machi 6,2014

No comments:

Post a Comment