Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, May 15, 2014

BASI LAGONGA LORI NA KUUA WATU 10 PAPO HAPO, LILIKUWA LIKITOKA MWANZA KWENDA BUNDA


WATU 10 wamekufa na wengine 10 kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria walilokuwa wakisafiria kugonga lori lililokuwa na kokoto lililoegeshwa kando ya barabara kisha kupinduka katika eneo la Nyamhongholo, jijini Mwanza.
 Akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya Rufaa ya Bugando, Daktari wa Idara ya Dharura, Dk Regina Mutayangulwa, alisema miili ya abiria hao na majeruhi walipokewa hospitalini hapo juzi usiku.
Majeruhi waliolazwa katika wodi za upasuaji ni pamoja na wanawake watatu waliolazwa katika wodi namba 9C na wanaume saba waliolazwa katika wodi namba 6Cna 8E na hali zao zinaendelea vizuri.
Waliojeruhiwa ni pamoja na Verynice Protas (22), Rosemary Petro (26), Prisca Peter (25), Hamad Haruna (22) ambaye amevunjika mkono wa kushoto na paji la uso kuharibika na Benson Joseph (27).
Wengine ni Nyanda Sahani, Magesa Musa (30), Rushinge Nyerere, Japhet Mlangwa (23) na Shija Nyanda Ngwenda.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentine Mlowola, alisema ilitokea Mei 13 saa moja usiku katika Barabara Kuu ya Mwanza- Musoma.

Alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye usajili namba T 769 CQE aina ya Toyota Coaster, lililokuwa likiendeshwa na Yohana Mayandakia likitokea Mwanza kwenda Bunda, ambapo liligonga  Lori aina ya Iveco, lenye namba T832 AEF na tela namba T 187 AEF.

Alisema lori hilo lilikuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara na dereva aliyeitwa Emmanuel Zakaria (33) ambalo lilikuwa bovu.


Kamanda Mlowola alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kutokuwa mwangalifu na ishara iliyokuwa imewekwa mbele ya gari lililokuwa bovu. Dereva wa lori anashikiliwa  na  Polisi kwa uchunguzi zaidi.

No comments:

Post a Comment