Hayo
yamo katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira kuhusu bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Bunge
limesisitiza kuwa jengo la ghorofa 16 lililoko katika Mtaa wa Indira
Gandhi, Dar es Salaam ambalo liliagiza mwaka jana livunjwe, agizo hilo
litekelezwe.
Aidha, imeishauri Serikali kutaifisha maeneo yote makubwa yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wananchi kwa matumizi mengine.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) akisoma taarifa
hiyo bungeni jana, alisema, “suala hili tuliliagiza katika bajeti
iliyopita na tunazidi kusisitiza utekelezaji huu ufanyike mara moja.”
“Kamati
inasikitikishwa kwamba agizo hili halijatekelezwa. Kamati inaiagiza
Serikali kulifikisha suala hili kwa Rais haraka ili lipatiwe ufumbuzi
kabla ya madhara kutokea,” alisema Bulaya.
Kuhusu ardhi, ilishauri
Serikali kuondoa mianya inayotoa fursa na ushawishi mbovu kwa viongozi
na watu wachache wasio na nia njema kwa maslahi ya Taifa, bali
kujilimbikizia mali kwa maana ya Taifa kwa kutumia mgongo wa Serikali.
“Aidha,
Kamati inaishauri Serikali kutaifisha maeneo yote makubwa
yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wananchi kwa matumizi mengine,” alisema
Bulaya.
Kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kamati iliishauri
Serikali kupitia Wizara ya Fedha ione umuhimu wa kuondoa Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) kwa nyumba zinazojengwa na shirika kwa ajili
ya kuuza kwa wananchi wa kipato cha chini na kati.
Pia, ilisema licha
ya Serikali kuondoa VAT na ushuru wa Forodha kwa shirika NHC kwa vifaa
vya ujenzi inavyoagiza nje, inaishauri kuliondolea pia shirika hilo VAT
kwa vifaa vya ujenzi vinavyozalishwa nchini.
Aidha, imeitaka Serikali
kulipa deni lililobaki la Sh 4,226,957,203.65 kwa NHC kutokana na
madeni ya Wizara, Taasisi na Idara za Serikali.
No comments:
Post a Comment