Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema hayo juzi usiku
wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa
mwaka wa fedha 2014/15.
Wakazi wa eneo hilo, wameshauriwa kuendelea
kuwa wavumilivu na kutokubali kurubuni wa kwa kuuza maeneo yao kwa
wajanja, ambao inaelezwa baada ya viwango vya fidia kutajwa,
wamejitokeza wakitaka kununua ardhi kwa bei poa, baadaye wafidiwe.
“Itambuliwe
kuwa viwango vya fidia katika Awamu ya Kwanza ya Mradi ni shilingi
35,000 kwa meta za mraba sawa na shilingi 141,645,000 kwa ekari moja.
“Hiki
ni kiwango kwa mujibu wa sheria kulingana na soko na thamani ya ardhi
itakavyokuwa katika mji mpya. Watu wanasema mimi ni wakala wa viwanja
Kigamboni, mimi ni Waziri wa Ardhi,” alisema Profesa Tibaijuka aliyeomba
aidhinishiwe bajeti ya Sh bilioni 88.8.
Aliwatoa wasiwasi watu
wanaodhani kuwa mradi huo umeshindikana. Alisisitiza kwamba viwango vya
fidia ni vizuri, kulingana na soko na thamani ya ardhi.
Aliwataka
wananchi wa Kigamboni kuwa na uvumilivu na imani na mradi huo, na
kuwashukuru kwa uvumilivu na ushirikiano wao wa kutambua azma ya
Serikali ya kujenga Mji Mpya mwenye viwango.
“Jambo hili ni gumu na
linachukua muda, lakini hatua iliyofikiwa si haba kwa zoezi lenyewe.
Niondoe wasiwasi kwa wale ambao wanadhani kwamba kazi hii imeshindikana
na hivyo tuondokane nayo.
“Mradi huu umetajwa kwa jina katika Ibara
ya 60(b)(iv) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2010
ambayo inaahidi ‘Kuanzisha Mji Mpya wa Kisasa wa Kigamboni (Kigamboni
New City.’
“Hii ni ishara tosha kuonesha wajibu wa Serikali katika
kutoa kipaumbele kutekeleza kazi hii,” alisema Profesa Tibaijuka na
kuongeza, “kwa hiyo, mimi nasonga mbele.”
Alisema ukosefu wa fedha
umechelewesha mradi, lakini hata hivyo, wamekamilisha uandaaji wa rasimu
ya muundo wa Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni (KDA) na
kuanzisha ofisi eneo la mradi.
Alisema Machi 2014, aliteuliwa
Mtaalamu wa Fedha na sasa ameanza kazi, jambo linalotarajiwa kuongeza
kasi ya kupata fedha za kutosha za utekelezaji wa mradi huo.
Kuhusu
fidia, alisema, “Naomba nirudie kwamba ili kulinda maslahi ya wananchi,
viwango vya fidia vilivyopangwa ni endelevu na wakati ukifika umahiri na
umuhimu wake utaonekana.”
Alisema tayari kuna wataalamu kutoka
Serikali ya Watu wa China ambao wamewasili kwa nia ya kushirikiana na
wataalamu wa ndani katika kupanga Mji Mpya wa Kigamboni na miji ya Lindi
na Mtwara.
“Wizara ina imani kuwa utaratibu huu wa kupata fedha za
kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni ukikamilika, mambo mengi ya mwanzo
yatapungua na kasi ya utekelezaji wa mji huo itaongezeka,” alisema
Profesa Tibaijuka.
Katika maoni yake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira, alitaka Serikali iwashirikishe wananchi
wa Kigamboni katika kila hatua ya utekelezaji, ikiwa ni pamoja na suala
la fidia.
“Kamati pia inaiagiza Serikali baada ya kuwepo kwa
ucheleweshaji mkubwa katika utekelezaji wa Mradi wa Mji Mpya wa
Kigamboni, ni wakati mwafaka sasa kubadili mkakati wa utekelezaji kwa
kushirikisha wabia wengine na wakiwemo wananchi wa Kigamboni,” ilisema
taarifa ya Kamati iliyosomwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya
(CCM).
Nayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ilihoji kama mpango huo
umefuata sheria kwa kiwango gani, kwani kumekuwa na malalamiko mengi.
No comments:
Post a Comment