GARI la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, limekamatwa na kuendelea kushikiliwa mjini Mombasa nchini Kenya, kutokana na kuwa na namba mbili.

Taarifa kutoka Kenya zilizolifikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa polisi nchini Kenya walipata taarifa za kuwepo kwa gari hilo na watu ambao walionekana kutokuwa na kazi maalumu.

Baada ya kupata taarifa hizo, Polisi hao walio katika msako wa wageni na magari yanayotiliwa shaka kuhusika katika uhalifu na ugaidi, walianza kulifuatilia na kubaini wahusika wa gari hilo.

Ufuatiliaji huo kwa mujibu wa taarifa hizo, ulibaini wahusika wa gari hilo walipofika Mombasa kutokea Tanzania, hawakuonekana kupokewa na mwenyeji yeyote, hali inayomaanisha wenyewe ni wenyeji wa mji huo.

Taarifa za Polisi zilibainisha kuwa uchunguzi wao ulibaini kuwa gari hilo liliwabeba Mbowe, Mbunge wa Mwanza Mjini, Ezekiah Wenje na dereva Ibrahim Nguzo.

Polisi hao inadaiwa walitilia shaka gari hilo kutokana na kuwa na namba za usajili STK 8146, ambazo zilipandishiwa juu ya nambari halisi za gari hilo ambazo ni KUB.

Uchunguzi wa Polisi hao ulibaini kuwa Mbowe na Wenje waliwasili Mombasa, Kenya kwa gari wakitokea Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro/Lungalunga na kwenda moja kwa moja hotelini.

Mashaka kwa Polisi hao yaliongezeka baada ya Mbowe na Wenje Aprili 26 mwaka huu kusafiri kwenda Nairobi kwa ndege, na kumwacha dereva pamoja na gari hotelini.

Kutokana na hali hiyo, Jumatatu wiki hii saa 5.00 asubuhi askari Polisi wa Mombasa walimkamata Ibrahim pamoja na gari hilo, baada ya kuonekana amekaa hotelini muda mrefu bila ya shughuli zozote.

“Hapo ndipo alipotoa habari kwamba alikuwa akiwasubiri wakubwa zake ambao walikwenda Nairobi tangu Aprili 26 na hawakuwa wamerejea,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ibrahim alipoulizwa kwa nini gari lilikuwa na nambari za kupandishiwa, alijibu huo ulikuwa ni uamuzi wa bosi wake Mbowe.

Polisi hao waliamua kukamata gari hilo na kulipeleka katika kituo cha Polisi cha Kati kwa mahojiano zaidi na baada ya mahojiano, aliachiliwa Ibrahim huru lakini gari limeendelea kuzuiliwa kituoni hadi Mbowe na Wenje watakapofika kwa ajili ya kuhojiwa.

Juhudi za kumtafuta Mbowe na Wenje hazikufanikiwa baada ya simu zao kutokupatikana.


CHANZO: Habarileo.