Wizara hiyo inayohudumia jeshi la
Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji
kupitia kwa Waziri wake, Mathias Chikawe, jana iliomba Bunge liidhinishe
bajeti ya Sh 881,740,291,800 kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi
ya kawaida na miradi ya maendeleo. Kiwango hicho kimetajwa kuwa ni kidogo
ikilinganishwa na majukumu ya wizara hiyo.
Wabunge mbalimbali waliochangia, ikiwemo
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Anna Abdallah,
walieleza kusikitishwa na kitendo cha wafungwa kupangiwa Sh 500 kwa siku kwa
kusema kibinadamu si sahihi kumlisha mtu kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya
milo mitatu.
Licha ya kusisitiza posho ya wafungwa
iongezwe hadi Sh 3,000 kwa siku, wabunge hao hasa kamati, pia walisisitiza
serikali iongeze posho ya chakula kwa askari wote chini ya wizara hiyo kutoka
Sh 5,000 hadi Sh 7,500 kwa siku.
Akisoma taarifa ya kamati, Hilda Ngoye
alisema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa
majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2013/14 pamoja
na maoni kuhusu makadirio na mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Kwa mujibu wa Ngoye, maelezo ya serikali
ni kwamba katika mwaka wa fedha 2013/14,
kiwango cha posho kwa wafungwa kilibaki kile kile cha Sh 500 kwa siku
kutokana na ufinyu wa bajeti. “Na kwamba hali itakuwa vivyo hivyo kwa mwaka wa
fedha 2014/2015,” alisema Ngoye.
Pia kwa upande wa posho ya askari,
alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014, kamati ilishauri posho hiyo iongezwe
lakini haikuongezwa.
“Kamati inazidi kuisisitiza serikali
kuwa Sh 5,000 kwa siku ni ndogo kwa kuzingatia gharama halisi ya chakula na
aina ya kazi wanazofanya,” alisema.
Hata hivyo katika taarifa hiyo ya bunge,
imeelezwa maelezo yaliyotolewa na serikali juu ya suala hilo ni kwamba wizara
imekamilisha taratibu za kuomba nyongeza hiyo ya posho kwa askari na kuwasilisha mapendekezo katika
Tume ya Rais ya Menejimenti ya Utumishi
wa Umma kwa hatua zaidi kabla ya kuwasilishwa Hazna.
Akichangia, Mbunge wa Vunjo, Augustine
Mrema alisema haiwezekani polisi akaishi kwa Sh 5,000 ya chakula kwa siku.
Alihoji kama wanafunzi wa vyuo vikuu
wanapangiwa posho ya Sh 10,000 kwa siku, iweje polisi apewe Sh 5,000 kwa
siku.
Mrema alikosoa pia hatua ya wafungwa kupangiwa bajeti ya Sh 500
kwa siku na kusema huo ni ukiukaji wa haki za binadamu.
“Mfungwa asihukumiwe kwa kunyimwa
chakula,” alisema na kushauri kamati ya ulinzi kukutana leo na Kamati ya Bajeti
kubadilisha viwango hivyo vya posho.
Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) alihoji vigezo vilivyozingatiwa kupangia wafungwa Sh
500 za chakula kwa siku. Alisema kuridhia wafungwa waendelee kupangiwa bajeti hii ni kutowatendea haki na
ni laana kwa Mungu.
Mbunge wa Kuteuliwa, Anna Abdallah
alitaka wabunge kuhakikisha wanaibana
Serikali wizara hiyo ya Mambo ya Ndani ya Nchi iongezwe fedha imudu
kutekeleza mahitaji yake, ikiwemo kuboresha hali ya maisha ya askari.
Katika majumuisho yake, Chikawe
alikubaliana na hoja nyingi za wabunge, ikiwa ni pamoja na bajeti ya mlo wa
wafungwa, akisema wameomba Hazina kiwango kipande na kufikia Sh 3,000 kwa siku,
na kama ikishindikana, kiwe Sh 1,500 kwa siku kama ilivyokubaliwa mwaka wa
fedha uliopita. Kwa upande wa posho za askari, alisema wameomba kiwango
kipandishwe na kufikia Sh 8,000 kutoka Sh 5,000 ya sasa.
No comments:
Post a Comment