Bunge
linaendelea na mkutano wake wa 15 mjini Dodoma leo, huku shughuli kubwa wiki
hii ikiwa ni kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali ya matrilioni ya shilingi.
Bajeti hiyo ni
ya mwaka wa fedha 2014/15. Pia, wiki hii kutafanyika uchaguzi wa wawakilishi wa
Bunge katika taasisi mbalimbali.
Kuhusu Bajeti
Kuu ya Serikali, Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya alieleza Aprili 30, mwaka
huu kuwa Serikali imepanga kutumia Sh trilioni 19.7 katika mwaka wa fedha wa
2014/15 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo.
Mkuya alisema
hayo jijini Dar es Salam, wakati akiwasilisha Mpango wa Bajeti ya mwaka ujao wa
fedha kwa wabunge.
Alisema kati ya
fedha hizo, fedha za matumizi ya kawaida ni
Sh trilioni 14.2 na zilizosalia ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Sh trilioni 14.2 na zilizosalia ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Waziri wa Fedha
alisema katika matumizi ya maendeleo, Serikali imeweka kipaumbele katika maeneo
sita ya kilimo, elimu, maji, nishati,
utafutaji rasilimali fedha na uchukuzi ikiwemo reli, barabara, madaraja,
magati, bandari, usafiri wa majini na usafiri wa anga.
Kwa mujibu wa
ratiba ya Bunge, Waziri wa Fedha atasoma Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali Juni
12, mwaka huu saa 10:00 jioni; na siku inayofuata pamoja na siku za mwisho wa
wiki, wabunge watasoma na kutafakari hotuba hiyo.
Kwa mujibu wa
ratiba hiyo, mjadala kuhusu bajeti hiyo, utachukua siku saba, ambapo utaanza Juni
16 hadi Juni 24, mwaka huu.
Bajeti ya sasa
utekelezaji wake unaishia Juni 30, mwaka huu, ambapo Serikali ilipanga kutumia
Sh trilioni 18.2. Tayari Serikali imekutana na baadhi ya washirika wa maendeleo
kwa siku mbili mjini hapa, kwa lengo la kuwataka waeleze utekelezaji wa
ahadi zao za kuchangia bajeti ya Serikali, kwa mwaka unaoishia Juni 30, mwaka
huu. Nchi ya Japan imeshatangaza kuwa itatekeleza ahadi yake.
“Tutakuwa na
mkutano washirika wa maendeleo hapa Dodoma kwa siku mbili kuanzia kesho.
Tutajadiliana na kuwaomba wakamilishe ahadi zao kabla ya tarehe 30 Juni
mwaka huu,” alisema Waziri wa Fedha, bungeni Alhamisi iliyopita.
Mkuya aliahidi
kuwa wizara yake, itatafuta fedha kutoka katika mafungu na vyanzo vingine ili
kuzipeleka katika wizara ambazo zilipata fedha pungufu ya zile zilizoidhinishwa
bunge mwaka jana.
Baadhi ya wizara
hizo ni Nishati na Madini, Maji, Uchukuzi, Afya na Ustawi wa Jamii na Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia.
Baadhi ya wizara
hizo zimepata kati ya asilimia 20 na asilimia 30 ya fedha zilizoidhinishwa
mpaka kufikia Aprili mwaka huu, ikiwa imesalia miezi miwili kumalizika kwa
mwaka wa sasa wa fedha.
Kwa mfano, hadi
kufikia Aprili mwaka huu, Serikali ilikuwa imeipatia Wizara ya Maji Sh
bilioni 39.4 tu zilizoidhinishwa na bunge. Fedha hizo ni sawa na asilimia 28 tu
ya kiasi kilichoidhinishwa. Fedha hizo pia ni sawa na upungufu
wa Sh bilioni
98.9.
Serikali
inatazama upya bajeti za wizara zote ili kutafuta vyanzo vingine vya fedha
za kupeleka katika wizara, ambazo bajeti zake zina upungufu.
Kinachofanyika
sasa ni Serikali kupata karibu Sh trilioni 1.8 ambazo zimepungua katika bajeti
kuu ya mwaka jana ya Sh trilioni 18.2.
Kuhusu
maandalizi ya Bajeti ya 2014/15, tayari Serikali
imeanza kufanya mashauriano ya siku sita na Kamati
ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Lengo la mashauriano hayo ni kufanya majumuisho na kuzingatia
hoja zenye maslahi ya Taifa, zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti za wizara
moja moja. Majadiliano hayo yanahudhuriwa pia na wenyeviti wa Kamati zote
za Kudumu za Bunge.
Kwa upande wa uchaguzi wa wawakilishi wa
Bunge, kwa mujibu wa Naibu Spika, Job Ndugai, tarehe ya mwisho ya
kurejesha fomu kwa wanaotaka kugombea ni Juni 8, mwaka huu saa 10:00 jioni.
“Nawatangazieni chaguzi mbalimbali
zitakazofanyika. Wale ambao mtapenda kushiriki, chukueni fomu kwa Katibu wa
Bunge kuanzia Juni 4 hadi Juni 8, mwaka huu saa 10,00 jioni,” alisema Naibu
Spika, Job Ndugai Juni 4, mwaka huu alipotoa matangazo bungeni.
Nafasi hizo za uwakilishi ni kundi la kwanza ni
wajumbe wa Bodi ya Mabaraza ya Vyuo Vikuu. Vyuo vikuu vya Serikali ni pamoja na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu
Mzumbe (MU), Chuo Kikuu Cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu Cha
Mbeya cha Sayansi na Teknolojia (MIST).
Ndugai alisema Kundi la pili ni Mwakilishi wa
Bunge katika mabunge ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC). Nafasi ipo wazi kutokana na aliyekuwa mwakilishi, Dk Titus Kamani
kuteuliwa na Rais hivi karibuni kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Kundi lingine ni Mwakilishi katika Tume ya Utumishi
wa Bunge, kutokana na aliyekuwepo, Godfrey Zambi kuteuliwa na Rais hivi
karibuni kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
No comments:
Post a Comment