Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema,
ameteleza ulimi tena na mara hii amejikuta akimuita Mbunge wa Kigoma Kusini,
David Kafulila (NCCR-Mageuzi) tumbili.
Kabla ya kutoa kauli
hiyo, Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Kafulila, kuhusu
fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), ambazo zimelipwa kwa kampuni ya PAP, inayomiliki mitambo ya kampuni ya
umeme ya Independent Power Tanzania Limited(IPTL).Werema alisema fedha hizo si
za Serikali, kama inavyodaiwa na Kafulila, kwa kuwa fedha za Serikali, hazikai
katika akaunti hiyo.
Alifafanua kuwa
taarifa zinazotolewa, zinapotosha
umma kuwa serikali imetoa fedha kuilipa IPTL,
wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo, kutokana na
misuguano baina ya wanahisa wawili, waliokuwa wamiliki wa IPTL.
Werema alibainisha
kuwa mmoja wa wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe, huku mwingine
akipinga jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na kumaliza mgogoro huo, ambapo
Mahakama iliruhusu mali za kampuni hizo,
apewe mwanahisa mpya, PAP.
Werema alisema kuna
watu walileta bungeni vipeperushi,
wakidai ni ushahidi kuhusu utoaji wa fedha hizo za akaunti ya Escrow na
kuhusisha na rushwa.
"Kafulila ni
miongoni mwa wanaoeneza taarifa
potofu…kama ni tuhuma au kuna rushwa, itakuja kujulikana, tusubiri uchunguzi wa
vyombo husika,” alisema.
Wakati akizungumza,
Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema kuwa wana usemi
unaosema kwamba 'Tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni'.
Kabla ya kufafanua
maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti, alikuwa akipiga kelele
kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa, hivyo atangaze maslahi yake.
“Naomba nisikilize,
hata kama ni mtuhumiwa, nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize wewe tumbili,”
alijikuta akisema Werema.
Baada ya kusema
hivyo, Kafulila hakukubali ;na yeye bila kuwasha kipaza sauti, alisema: “Wewe
(Werema) ni mwizi tu.”
Kutokana na hali
hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan 'Zungu' alimuomba Jaji Werema, kukaa
chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) na
Kafulila wakitaka kuzungumza.
Zungu alisema kwa
kuwa Bunge, lilishaamua kuwa suala hilo, lipelekwe Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), ni vyema kama Kafulila ana ushahidi wowote, apeleke huko.
Baada ya kutoa
mwongozo huo, ambao ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu alisitisha shughuli
za Bunge mpaka jioni na kuondoka, huku akisindikizwa na makatibu wa Bunge na
wapambe kama kawaida.Hatua ya Mwenyekiti wa Bunge kuondoka katika ukumbi, baada
ya kusitisha shughuli za Bunge, ilimpa fursa Jaji Werema kuweka sawa makabrasha
yake na kutoka katika kiti chake, ambapo alionekana kama vile anakwenda
kumkabili Kafulila.
Wakati hilo likitokea, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester
Kasulumbayi (Chadema), alihama katika kiti chake na
kukimbilia alipokuwa amekaa Kafulila.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mawaziri walimzunguka Jaji Werema, kabla hajamfikia
Kafulila na Kasulumbayi.
Mawaziri hao ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa
Sheria na Katiba, Dk Asha Rose Migiro na Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk
Abdullah Juma Abdullah Saadalla.
Nje ya Bunge, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na
waandishi wa habari, ambapo walidai kuwa na ushahidi wa kutuhumu baadhi ya
mawaziri, kusema uongo bungeni kuhusu fedha hizo za Escrow.
Credit: Habari leo
No comments:
Post a Comment