Dar es Salaam. Emmanuel Mbasha, ambaye ni mume wa mwimbaji
nguli wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha amejitokeza hadharani na kusema kwamba
atakwenda polisi mwenyewe kujibu tuhuma dhidi yake za kumbaka shemeji yake
mwenye umri wa miaka 17.
Faili la tuhuma dhidi ya Mbasha lilifunguliwa Jumatatu iliyopita
katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule) wakati shemejiye huyo (jina
tunalihifadhi), alipotaarifu kuwa Mbasha alimbaka mara tatu kwa siku mbili
tofauti. Kesi hiyo ilipewa namba TBT/RB/3191/2014 na TBT/IR/1865/2014.
Tangu siku hiyo, polisi imekuwa ikieleza kuwa inamsaka
Mbasha bila ya mafanikio lakini mwishoni mwa wiki mtuhumiwa huyo aliongea na
gazeti hili na kuelezea upande wake wa tukio hilo na kwamba yuko tayari
kujisalimisha ili ukweli ubainike.
“Tuhuma dhidi yangu ni za kutengeneza,” alisema Mbasha na
kufafanua kuwa yote hayo yanatokana na mgogoro wa kifamilia baina yake na Flora
na familia yake ambao alisema umedumu kwa siku kadhaa.
“Mimi sijabaka na sijawahi kubaka; sijatenda dhambi yoyote;
sijafanya kitu chochote na kibaya haya mambo yote ni ya kusingiziwa tu. Mungu
wangu ni shahidi. Na kwa kuwa sijafanya hiyo dhambi kama wanavyodai, basi Mungu
wangu atanitetea,” alisema Mbasha ambaye anaonekana zaidi kwenye video ya wimbo
wa Maisha ya Ndoa alioshirikiana na mkewe Flora.
“Si wamesema wananitafuta, nitakwenda mwenyewe polisi.
Nitawasikiliza na nitatoa maelezo yangu. Kama wakinipeleka mahakamani basi
ukweli utajulikana... ipo siku kila kitu kitakuwa wazi.”
Kabla ya kufunguliwa kwa faili la tuhuma hizo, msichana huyo
alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Ilala (Amana) ambako alifunguliwa
faili la matibabu namba 667. Matokeo ya vipimo ambavyo vilifanywa na daktari
kung’amua kama binti huyo aliingiliwa vinaonyesha kuwa kulikuwa na mbegu
utokaji wa mbegu usio wa kawaida (HVD).
Kadhalika binti huyo
alifanyiwa vipimo kuona kama ameambukizwa virusi vya Ukimwi (VVU), pia kupata
ujauzito, lakini matokeo ya awali yalionyesha kuwa yupo salama.
Akiwa nje ya kituo cha polisi Jumatatu usiku, binti huyo
aliliambia gazeti hili kwamba mara ya kwanza alibakwa mchana Mei 23 na kwamba
mtuhumiwa alirudia kitendo hicho Jumapili Mei 25 usiku ndani ya gari katika
eneo la Tabata, ambako anadai alifanyiwa kitendo hicho mara mbili.
Hata hivyo, Mbasha alihoji: “Hivi kweli hata kama mimi ni
mbakaji, kweli nimbake mtoto wa kumlea mwenyewe mara tatu, yaani Ijumaa halafu
nirudie tena Jumapili? Hata kama ni kusingiziwa basi tuhuma hizi zimezidi.”
“Huyu binti nimekaa naye miaka mingi na sijawahi kumfanyia
hivyo. Hapo nyumbani kwangu wamekaa mabinti wengi, wakiwamo shemeji zangu
wadogo zake na Flora na sikuwahi hata kuwagusa, leo hii kwa nini wananifanyia
hivi?”CHANZO MWANAINCHI
No comments:
Post a Comment