Katika toleo Na. 1734 la gazeti la Jambo Leo la tarehe 10
Juni, 2014 katika ukurasa wa tatu
iliandikwa taarifa iliyokuwa na kichwa cha habari “Utafiti wa gesi kuinufaisha Morogoro,
Kilimanjaro”. Taarifa hiyo ilieleza kuwa
wakaazi wa mikoa tajwa watanufaika na ugunduzi wa mafuta na gesi
uliofanywa na Kampuni ya Swala katika
maeneo hayo. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linapenda
kuwafahamisha wananchi kuwa taarifa ya
kwamba Kampuni ya Swala imegundua
gesi na mafuta katika maeneo ya Morogoro na Kilimanjaro sio
sahihi. Ugunduzi wa mafuta hufanyika tu
baada ya kuchimba kisima cha utafiti na hatimaye mafuta au gesi iweze kutoka yenyewe kutoka ardhini.Hatua ya
kuchimba kisima cha utafutaji hutokana
na tafiti mbali mbali za awali za mitetemo ya ardhi na kubaini kama maeneo hayo yana uwezekano wa kuwa na mafuta
au gesi ama la. Hata kama eneo
linaonesha dalili nzuri za awali ni lazima sehemu hiyo ichimbwe na matokeo yake ni kuwa na ugunduzi au la. Vilevile
ugunduzi huo lazima uonyeshe kutoa kiasi cha rasilimali ambacho kinaweza
kuzalishwa kibiashara (economically
viable).
Kazi zilizofanyika mpaka sasa na Kampuni ya Swala katika
maeneo ya Morogoro – Kilosa na Pangani
- Kilimanjaro ni utafiti wa awali wa kukusanya takwimu za mitetemo na kubaini kama maeneo hayo yana
kina (thickness) cha kutosha cha miamba
tabaka ambayo utafiti wa mafuta na gesi unaweza kufanyika. Hivyo utafiti wa kina unaendelea ili kubaini kama
kuna miamba mashapo (prospects) ya
kutosha kwa ajili ya kuchimba kisima cha utafiti. Uchimbaji wa kisima
hicho unaweza kutoa mafuta au/na gesi au
maji matupu. Hatua ya uchimbaji visima
bado haijaanza.Hivyo basi si sahihi kwa mtu yeyote kusema kuwa kuna ugunduzi uliofanyika.
Utaratibu wa kutafuta mafuta nchini ni wa kugawana mapato
kati ya Mwekezaji na Serikali kupitia
Mikataba ya Kugawana Mapato (Production Sharing
Agreement-PSA) kama mafuta au gesi ikigundulika. Kampuni isipogundua rasilimali yeyote, Serikali haimrudishii
Mwekezaji fedha zake alizowekeza kwenye ufafiti
huo, hivyo hasara hiyo ni kwa Mwekezaji mwenyewe.
Shirika lina taarifa kuwa Kampuni ya Swala inauza Hisa zake
katika soko la Hisa la Dar es Salaam ili
Watanzania washiriki katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi. Suala hili ni jema na Kampuni ya
Swala inastahili kupongezwa kwa
kuwawezesha Watanzania kushiriki kwenye sekta hii ambayo imeshika kasi
katika miaka mitatu iliyopita. Aidha,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
linawashauri Wananchi wafanye maamuzi mazuri na kuwatumia washauri
wao kuhusu ununuzi wa hisa hizo kwa
kuzingatia mambo yaliyoelezwa hapo juu. Ikumbukwe kuwa Tanzania tumechimba
visima vya utafiti wa mafuta vipatavyo
78 na vyenye gesi ni asilimia 40% tu huko Mkuranga (Pwani),
Songosongo (Lindi), Ntorya na Mnazi Bay
(Mtwara) na Bahari ya kina kirefu. Taarifa
kuwa katika mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro kumefanyika ugunduzi wa mafuta na gesi haina ukweli wowote. Kama
rasilimali ya mafuta au gesi asilia
ikigundulika mwenye mamlaka ya kutangaza ugunduzi huo ni Mheshimiwa
Waziri wa Nishati na Madini pekee.
Kwa maelezo zaidi
wasiliana na: - Mkurugenzi Mtendaji,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania,
BWM Tower A,
S.L.P 2774,
Dar es Salaam.
Barua pepe: tpdcmd@tpdc-tz.com
No comments:
Post a Comment