Hatimaye
Malawi imempata Rais wake mpya, baada ya mivutano ya kisheria iliyoibuka mara
baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Mei 20, mwaka huu.
Msomi
mahiri wa masuala ya sheria, Profesa Arthur Peter Mutharika anayekiongoza Chama cha
Democratic Progressive (DPP), ndiye aliyetangazwa kuwa Rais wa Tano wa Malawi.
Profesa Mutharika ni mdogo wa aliyekuwa Rais wa Tatu wa nchi hiyo, Bingu wa
Mutharika.
Katika
matokeo rasmi ya uchaguzi huo yaliyotangazwa juzi usiku na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ya Malawi (MEC), Mutharika ameshinda baada ya kupata asilimia 36.4 za
kura zote, na hivyo kumng’oa rasmi Rais Joyce Banda aliyekuwa anawania tena
nafasi hiyo.
Mutharika
aliapishwa jana asubuhi katika Mahakama Kuu ya Blantyre, huku akiwaasa raia wa
Malawi kushirikiana naye katika kuijenga nchi, kwani kipindi cha malumbano na
kampeni za kisiasa kimeshaisha huku akisisitiza kuijenga Malawi.
Hata hivyo,
tofauti na wiki iliyopita alipotangaza kufuta uchaguzi mkuu na kuyakataa
matokeo yote, akitaka urejewe baada ya siku 90, jana Rais Banda aliibuka na
kumpongeza mshindani wake.
Aidha, Banda
aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo, alitumia fursa hiyo kuwasihi
wafuasi wake kukubaliana na matokeo, akisema hivyo ndiyo demokrasia.
Kwa mujibu wa
MEC, Mchungaji Dk Lazarus Chakwera ndiye aliyeshika nafasi ya pili ya kura
zote, akipata asilimia 27.8 huku Rais anayemaliza muda wake Dk Joyce Banda
akishika nafasi ya tatu kwa asilimia 20.2 na Atupele Muluzi amekuwa wa nne
akipata asilimia 13.7.
Awali Jaji
Kenyatta Nyirenda wa Mahakama Kuu mjini humo, juzi usiku alitoa uamuzi kuwa
hawezi kuvunja Sheria kwa kuruhusu tume iongeze muda wa kuhesabu upya kura
kwenye maeneo yenye utata na kwamba Sheria inaitaka tume kutangaza matokeo
ndani ya siku nane na si vinginevyo.
Matokeo hayo
yalitangazwa dakika chache baada ya mahakama kukataa kuongeza muda wa kuhesabu
kura upya, ambi ambalo lilitolewa na Chakwera.
Mtangazaji wa
Kituo cha Utangazaji cha Al Jazeera, Haru Mutasa katika mji wa Blantyre,
alisema Mutharika alianza mchakato wa kuapishwa mapema jana ili kukwepa
kukabiliana na pingamizi.
Alhamisi,
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Maxon Mbendera, alisema uchaguzi wa Urais
ulikuwa huru na wa haki na ulifanyika katika mazingira ya uaminifu ingawa
kulikuwa na mambo yasiyokuwa ya kawaida yaliyogundulika katika zaidi ya vituo
4,000.
Malawi
ililazimika kupeleka jeshi siku ya kwanza ya uchaguzi wiki iliyopita baada ya
vituo vya kupigia kura kuchelewa kufunguliwa na kusababisha wapigakura kufanya
fujo na kuchoma vituo viwili.
Uchaguzi wa
Malawi ulifanyika Mei 20 nchini kote, lakini siku moja tu baada ya kupiga kura,
malalamiko yakiambatana na mapingamizi ya kisheria yakatawala kwenye Mahakama
Kuu za Lilongwe na Blantyre.
Banda alikuwa
miongoni mwa waliopinga, akienda mbali zaidi na kutangaza kusitisha shughuli
zote za uchaguzi huo.
Banda
aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka miwili kuanzia Aprili 7, mwaka 2012,
ikitangazwa anaelekea kushindwa katika uchaguzi huo, aliibuka na kuamuru
kusitishwa mara moja kwa shughuli ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya
uchaguzi huo mkuu wa nchi hiyo.
Akizungumza
katika Ikulu yake jijini Lilongwe mwishoni mwa wiki iliyopita, Banda mwenye
umri wa miaka 64, aliiamuru MEC kusitisha shughuli hiyo na kutangaza uchaguzi
wa Rais, Wabunge na Madiwani utarudiwa ndani ya siku 90 kuanzia Jumamosi ya Mei
24, mwaka huu. Pia alitangaza kutogombea tena katika uchaguzi wa marudio.
Katika
maelezo yake, alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kwa kile alichokiita ni
kuvurugika kwa mtiririko mzima wa shughuli za upigaji kura, kuhesabu na hata
namna ya kusimamia utoaji wa matokeo yake. Kwa ujumla, ameuita ulikuwa uchaguzi
uliojaa 'mchezo mchafu’.
Lakini
uamuzi wa juzi wa MEC umekata mzizi wa fitina na kumaliza mivutano yote
iliyokuwepo, hivyo kumfanya Mutharika kuwa Rais wa Tano wa Malawi. Watangulizi
wake ni Hastings Kamuzu Banda aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka 27 na siku 319
kuanzia Julai 6, mwaka 1966.
Banda
alirithiwa na Bakili Muluzi Mei 21, 1994 na kuiongoza nchi kwa miaka 10 na siku
tatu. Bingu wa Mutharika aliongoza kwa miaka saba na siku 317. Alifikwa na
mauti akiwa madarakani, hivyo Joyce Banda aliyekuwa makamu wa Rais kukabidhiwa
kijiti kuanzia Aprili 7, mwaka 2012 hadi Mei 31, mwaka huu, ikimaanisha amekuwa
Rais wa Malawi kwa miaka miwili na siku 54.
Kwa
ushindi wa Profesa Mutharika katika kiti cha urais wa Malawi, anaongeza idadi
ya jamii ya wasomi waliopitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ama wakiwa
wahadhiri au wanafunzi, kwani alifundisha chuoni hapo mwishoni mwa miaka ya
1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970. Amefundisha pia katika Vyuo Vikuu vya Haile
Selassie (Ethiopia), Rutgers (Marekani), Makerere (Uganda), Washington
(Marekani) na pia ni mhadhiri anayefundisha kwa muda katika Shule ya Uchumi
London, Uingereza.
Nje
ya kazi za uhadhiri, Profesa Mutharika aliyebobea katika masuala ya sheria
ambaye pia ni mwanasiasa mzoefu na mashuhuri, ameshika nyadhifa za uwaziri
katika wizara mbalimbali zikiwamo Wizara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
nafasi aliyoishika hadi anaingia katika uchaguzi mkuu hivi karibuni.
Mbali ya
Profesa Mutharika, wasomi wengine waliopitia UDSM na kufanikiwa katika ulingo
wa kisiasa na hata kuwa marais au viongozi waandamizi katika nchi zao ni Rais
Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa zamani wa Zaire (sasa
DRC) Laurent Desire-Kabila.
Aidha, Makamu
wa Rais wa zamani wa Uganda, Eriya Kategaya alisoma Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, kama ilivyo kwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Sudan, John Garang.
Naibu Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ambaye kwa sasa ni Waziri wa
Sheria na Katiba, naye alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama ilivyo kwa
Mawaziri wakuu watatu wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba, Edward Lowassa na
Mizengo Pinda. Getrude Mongella, Rais wa zamani wa Bunge la Afrika ambaye pia
alishika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya
Wanawake Duniani uliofanyika Beijing, China mwaka 1995. Amewahi pia kuwa balozi
India, Waziri Asiye na Wizara Maalum, Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii,
mshauri maalum wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni
(UNESCO).
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa sasa wa Tanzania,naye amesoma Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam. Watu wengine mashuhuri waliosoma Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ni pamoja na mwanasheria Mkuu wa Kenya, Dk Willy Mutunga na Donald Kaberuka, Rais wa
Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambaye ni raia wa Rwanda.
No comments:
Post a Comment