Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imefungua
milango kwa mawaziri na wabunge kufunguliwa mashtaka kutokana na kauli
watakazozitoa bungeni ambazo ni kinyume cha Katiba na Sheria.
Mahakama Kuu ilitoa msimamo huo jana wakati ikitoa uamuzi wa
pingamizi la awali katika kesi ya kikatiba iliyokuwa ikimkabili Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, lililowasilishwa na Jopo la Mawakili wa Serikali wakiongozwa na
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG, George Masaju.
Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013 ilifunguliwa na Kituo cha
Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), aliyeunganishwa kama mlalamikiwa wa pili.
LHRC na TLS walikuwa wakidai kuwa Pinda alivunja Katiba
kutokana na kauli aliyoitoa bungeni, wakidai kuwa ni amri kwa vyombo vya
utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Hivyo, walikuwa wakiiomba mahakama, pamoja na mambo mengine,
itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha Katiba na imwamuru Pinda aifute
hadharani.
Hata hivyo, Pinda na AG waliokuwa wakitetewa na DAG Masaju
akisaidiana na Mawakili wa Serikali Wakuu (PSA, Gabriel Malata, Alecia Mbuya na
Sarah Mwipopo), waliweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo, wakitoa hoja
tano za kuomba kesi hiyo itupiliwe mbali.
Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kwamba kesi hiyo ni
batili na iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya Mwaka 1977 na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge, ya mwaka
1988.
Mawakili hao walidai kuwa Pinda analindwa na Katiba Ibara ya
100 (1) na (2), ambazo zinamkinga mbunge kushtakiwa au kufunguliwa shauri la
madai mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, au alilolitenda, au
alililoliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada au hoja.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake jana ilikubaliana na baadhi
ya hoja za mawakili wa utetezi (Serikali) na kuitupilia mbali kesi hiyo, lakini
ikatamka kuwa wabunge na mawaziri wanaweza kushtakiwa kwa kauli au jambo
walilolitamka bungeni, linalokiuka sheria na haki za binadamu.
Uamuzi huo ulisomwa na Kiongozi wa Jopo la Majaji wa
Mahakama Kuu, lililokuwa likisikiliza kesi hiyo, Jaji Kiongozi Fakih Jundu kwa
niaba ya majaji wenzake, Agustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.
Katika uamuzi huo, majaji walikubaliana na hoja tatu za
pingamizi kuwa walalamikaji katika kesi hiyo hawakuwa na haki ya kufungua kesi
hiyo na kwamba walikosea taratibu za ufunguaji wa kesi kama hizo kwa kuwa
walikiuka amri na kanuni zinazoongoza Mashauri ya Madai (CPC).
Katika hoja ya kwanza kuwa Pinda kama mbunge analindwa na
Katiba, jopo hilo lilisema kuwa ni kweli wabunge wanalindwa na Katiba Ibara ya
100 (1) kuhusu haki na upendeleo (Previledge), yaani haki na uhuru wa mjadala
na maoni. Hata hivyo, lilikataa hoja za utetezi kuwa wabunge wana kinga isiyo
na mipaka ya kutokushtakiwa kwa kauli au jambo lolote walilolitamka bungeni.
Badala yake jopo hilo lilikubaliana na hoja za mawakili wa
walalamikaji, kuwa japo wabunge wana kinga, lakini kinga yao ina mipaka na kwa
kuwa inadhibitiwa na masharti ya ibara nyingine za Katiba na Sheria za Bunge.
Walalamikaji walikuwa wakitetewa na Peter Kibatala, Fulgence
Massawe, Harold Sungusia, Mpale Mpoki na Jeremiah Mtobesya.
Kuhusu hoja ya pingamizi kuwa walalamikaji hawakuwa na haki
ya kufungua kesi hiyo, mahakama ilikubali kuwa kwa walalamikaji katika kesi
hiyo hawakuwa na haki ya kufungua kesi hiyo.
Ilifafanua kuwa anayepaswa kufungua kesi ni yule tu
aliyeathirika na kauli iliyotolewa na mlalamikiwa na si mashirika, kwa kuwa
kauli ya mlalamikiwa haikuyaathiri mashirika hayo yaliyofungua kesi.
Mahakama ilifafanua kuwa mtu aliyeathirika na kauli
iliyotolewa bungeni anaweza kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge hasa kanuni ya 71 (1) .
Ilisema kwa kuwa kanuni hiyo haitoi nafasi kwa mashirika,
basi mashirika yanaweza kufungua kesi mahakamani kwa kufuata taratibu za
kisheria, ikiwa kauli iliyotolewa bungeni itakuwa imeyaathiri moja kwa moja.
Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Kibatala alisema kuwa ingawa
kesi yao imetupiliwa mbali, lakini kitendo cha mahakama kutamka kuwa wabunge
hawana kinga isiyo na mpaka na kwamba wanaweza kushtakiwa ni ushindi mkubwa.
Kwa upande wake Wakili Sungusia alisema kuwa wiki ijayo
watakutana na jopo la mawakili ili kujadili uamuzi huo na hatua za kuchukua
kama watakata rufaa Mahakama ya Rufani au la.
Katika pingamizi lao, mawakili wa utetezi pia walidai kuwa
hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani haijasainiwa kwa kuwa waliosaini si
walalamikaji na kwamba hawajaonyesha kama wamepewa mamlaka ya kusaini kwa niaba
ya walalamikaji.
Walidai kuwa walalamikaji ni taasisi yaani LHRC na TLS,
lakini waliosaini ni Dk Hellen Kijo Bisimba kwa niaba ya LHRC na Wakili Francis
Stolla (Rais wa TLS) kwa niaba ya TLS, lakini hawaonyeshi kama wamepewa mamlaka
ya kusaini hati hiyo.
Pia mawakili wa walalamikaji walidai kuwa hati ya madai ina
dosari za kisheria kwa kuwa kwa mujibu wa kanuni za Uendeshaji wa Mashauri ya
Madai (CPC), hati inapaswa kueleza madai tu na si ushahidi, hoja wala maoni,
walalamikaji wameelezea na maoni yao binafsi.
Upande wa walalamikaji katika majibu yao walidai kuwa
walalamikaji wana haki ya kuwashtaki walalamikiwa. Wanadai kuwa kinga ya mbunge
ina mpaka na inamlinda kwa shughuli za bunge tu na kwamba hati hiyo haina
dosari huku wakidai kuwa hata kama zipo dosari za kisheria, basi zinaweza
kurekebishwa.
Pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa, katika mkutano wa
11 wa Bunge wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu
bungeni, Juni 20, 2013.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa
Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu kuhusu msimamo wa Serikali, pamoja na mambo
mengine, malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama
Mtwara, kuwapiga wananchi.
“Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi,
utapigwa tu... Eeh, hamna namna nyingine, eeh maana lazima tukubaliane kwamba
nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara
zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi... watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu,
kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh… maana tumechoka,” inasomeka hati ya
madai ikinukuu maneno ya Pinda.
MWANANCHI


No comments:
Post a Comment