Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimesema hakitasubiri wanachama watakaoachwa na Chama cha Mapinduzi (CCM)
kwenye uteuzi wa wagombea katika uchaguzi mkuu ujao.
Kutokana na tamaa ya kuingiza watu wengi kwenye Bunge, vyama
vya upinzani vimekuwa na tabia ya kuwapokea wanachama wa CCM wanaoshindwa
kwenye kura za maoni na baadaye kuwapa nafasi ya kugombea ubunge, lakini Dk
Slaa anasema safari hii hawatakuwa tayari kufanya hivyo.
“Tulishasema kwamba kwa
ngazi zozote hata ngazi za udiwani au ubunge hatusubiri mabaki, makapi
yatakayotokea CCM ndiyo yaje kwetu,” alisema Dk Slaa katika mahojiano maalumu
na Mwananchi yaliyofanyika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
“Safari hii hatusubiri. Tulishasema kuwa wagombea wetu
tunawaandaa mapema ili tusitegemee mtu anayekuja dakika za mwisho kuwa ndiyo
atuokoe.”
Kauli ya Dk Slaa inaweka msisitizo katika ile iliyowahi
kutolewa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwamba hawatapokea
wanasiasa watakaoihama CCM ili kupata nafasi za uongozi kwa tiketi ya Chadema.
Katika mahojiano hayo, Dk Slaa alisema: “Huwezi kuzuia
kupokea mwanachama kokote alikotokea, lakini unapofika wakati wa kuweka watu
katika nafasi, lazima ufikirie.”
Mwaka 2010, Chadema ilipokea wagombea wawili walioshindwa
kwenye kura za maoni za CCM, John Shibuda aliyeshindwa katika kura za maoni za
Maswa Magharibi na Freddy Mpendazoe ambaye alienguliwa kwenye kura za maoni za
CCM Jimbo la Segerea.
Shibuda alifanikiwa kurudi bungeni baada ya kushinda
uchaguzi wakati Mpendazoe alishindwa katika hali ya kutatanisha na juhudi zake
za kutengua matokeo hayo mahakamani ziligonga mwamba.
“Tatizo hilo lilitokana na ugeni wetu,” alisema Dk Slaa
akizungumzia kitendo cha Chadema kupokea wagombea walioshindwa CCM kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
“Lakini kwa wakati huu, Chadema ina wanachama wengi wenye
sifa za kugombea hivyo hatuhitaji kusubiri mtu,” aliongea katibu huyo mkuu
ambaye aliwahi kutangaza kuwa nafasi za wagombea ubunge wa Chadema katika
majimbo yote nchini zitatangazwa kwenye magazeti na watakaojitokeza,
watafanyiwa usaili.
Kuhusu uchaguzi mkuu wa chama hicho, Dk Slaa alisema
utafanyika Desemba mwaka huu baada ya kuridhiwa na kikao cha Kamati Kuu
kitakachofanyika Julai 18.
Alisema wanahakikisha uongozi unapatikana kuanzia ngazi za
chini na watachukua hatua kwa maeneo ambayo watabaini viongozi wamepeana
nyadhifa bila chaguzi madhubuti kufanyika.


No comments:
Post a Comment