WAZIRI Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
ameutaka uongozi mpya wa Klabu ya Simba kutolipiza kisasi au kufukua maovu ya
uongozi uliopita na badala yake kujikita katika kuweka mikakati ya kuendeleza
klabu.
Lowassa alisema hayo ofisini kwake Dar es Salaam jana
alipotembelewa na Rais mpya wa Simba, Evans Aveva. Lowassa amemtaka Aveva
kuunganisha wanachama wa Simba kwa manufaa ya soka la Tanzania
Aidha, aliwataka viongozi wa klabu kubwa nchini kusajili
zaidi wachezaji wa nyumbani na kuachana na tabia ya kukimbilia kusajili
wachezaji wa kigeni kwani hiyo inadhoofisha uimara wa timu ya taifa.
Lowassa alitolea mfano timu ya Taifa ya England ilivyofanya
vibaya katika fainali za Kombe la Dunia la Fifa akisema inatokana na klabu za
Ligi Kuu ya nchi hiyo kuwa na wachezaji wengi wa kigeni kuliko wa ndani.
Kwa upande wake, Rais huyo wa Simba, Aveva alisema uongozi
wake umejipanga kuwekeza katika vijana ili kupunguza gharama za kusajili
wachezaji wapya kila msimu.
Pia alimweleza Lowassa kuwa wanatarajia kufungua hosteli
katika kipindi kifupi kijacho katika eneo jipya la klabu hiyo Bunju katika
Manispaa ya Kinondoni.
Amesema awamu ya pili ndiyo itakuwa ya ujenzi wa uwanja
ambapo alimwomba Lowassa kukubali mwaliko wa kufanya harambee ya kukusanya
fedha za ujenzi wa uwanja huo wakati ukifika.


No comments:
Post a Comment