ZIARA
ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Taifa, Philip
Mangula mkoani Kigoma, imemponza Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya
Uvinza mkoani hapa, Majaliwa Zuberi na kujikuta akitupwa jela mwezi
mmoja.
Zuberi, alihukumiwa kifungo hicho na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo,
Kata ya Nguruka, wilayani Uvinza, William Mugisa kwa kosa la kudharau
mahakama.
Inaelezwa kuwa wakati mahakama ikiendelea na shughuli zake jana
asubuhi, Zuberi alikuwa akifanya maandalizi ya kumpokea Mangula kwenye
ukumbi wa CCM Social Hall ambao uko karibu na mahakama hiyo, kwa kupiga
nyimbo za kukisifu na kukipamba chama hicho.
Kutokana na kitendo cha kupiga muziki kwa sauti ya juu, Hakimu Mugisa
aliagiza akaitwe katibu huyo na kumtaka akazime nyimbo hizo kutokana na
kuingilia shughuli za mahakama na kumpa dakika tano akatekeleze, lakini
aliporejea ukumbini aligoma.
Kutokana na kukaidi amri hiyo, Hakimu Mugisa aliagiza askari
wakamkamate na kumpandisha kizimbani na kukumbana na adhabu hiyo ya
kwenda jela mwezi mmoja kutokana na kuidharau mahakama.
Chanzo:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment