Ofisi ya Ustawi wa Jamii katika halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga inafanya uchunguzi juu ya Ukatili aliofanyiwa Mtoto wa miaka Miwili Helena Joseph ambaye inadaiwa kuteswa kwa kuchomwa moto na Mama yake wa Kambo.Kwa mujibu wa afisa ustawi wa Jamii wa halmashauri hiyo Regina Nkwabi juhudi zinafanyika kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia ambapo anayetuhumiwa kufanya kitendo hicho Helena Paul anahojiwa kuhusu tukio hilo.Nkwabi amesema mtoto huyo kwa sasa anaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya ya Kahama, huku hali yake ikielezwa kuwa sio nzuri kutokana na kuwa na majeraha katika mwili wake na vidonda kichwani.
Amesema Taarifa za awali zinaeleza kwamba mtoto huyo ameonekana kuathiriwa kutokana na kupigwa mara kwa mara huku akichomwa moto katika mwili wake na kwamba wanasubiri taarifa kutoka katika hospitali ili kujua mtoto huyo amezidiwa kiasi gani.
Inadaiwa Mama mzazi wa mtoto huyo ambaye amefahamika kwa jina Moja la Nyamizi alimpeleka mtoto huyo kwa baba yake mzazi ambaye anaishi na Mke mwingine ambaye ndio mtuhumiwa ili aishi huko kutokana na kwamba yeye pamoja na mtoto walikuwa wagonjwa.
Waandishi wa habari waliambatana na dawati la Jinsia, ustawi wa Jamii pamoja na shirika lisilokuwa la kiserikali la kutetea haki za Binadamu wilayani Kahama SHIHABI, kwenda kumtafuta mama mzazi wa Mtoto huyo ambaye anaishi Bukondamoyo ambapo hakupatikana.
Mmoja wa Majirani wa mama huyo Matrida Lucas amesema mtoto huyo takribani wiki tatu wakati anapelekwa kwa baba yake alikuwa mgonjwa lakini hakuwa na majeraha kama aliyonayo kwa sasa.
Juhudi za kumtafuta baba mzazi wa Mtoto huyo Joseph Mkazi wa Bukondamoyo hazikuzaa matunda kutokana na kwamba amekwenda Porini kukata mkaa.
Katibu msaidizi wa Shirika la SHIHABI Mohammed Sukwa amesema Wataendelea kushirikiana na Usitawi wa Jamii kwa kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake kwa mtu atakayebainika anakosa kwani ni kinyume cha sheria za haki za Binadamu.
via>>Farajimfinanga.com
No comments:
Post a Comment