Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
amemtaka Rais Jakaya Kikwete kujitokeza hadharani kutafuta suluhu ya kupata
mwafaka wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hakuna mamlaka nyingine zaidi
inayoweza kuunusuru.
Pia, amewatahadharisha viongozi wa dini kuwa makini na kauli
zao wanazozitoa za kuwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kurejea bungeni Agosti 5.
Dk Slaa aliyasema hayo juzi katika mahojiano maalumu na
gazeti hili, makao makuu ya Chadema Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es
Salaam.
“Mwenye rungu la kuweza kutengua kitendawili hiki ili turudi
bungeni ni Rais (Kikwete) mwenyewe, hakuna mwingine,”alisema Dk Slaa.
“Tatizo aliyesaini waraka uliowasilishwa na Warioba ni Rais
mwenyewe, alisaini ukurasa wa kwanza na wa mwisho, kwa taarifa rasmi za kina
Warioba, Rais alishirikishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hatua kwa hatua na
kwa kila hatua alisema sawa mchakato uendelee,”alisema Dk Slaa.
Alikumbusha kuwa wakati akipokea Rasimu ya Pili ya Katiba,
Rais Kikwete alisema: “Mtapata rasimu, ijadilini na itapitishwa na Bunge. Kwa
mwanasheria yeyote, lugha kujadiliwa na kupitishwa haitoi ruhusa ya
kubadilishwa, inatoa ruhusa kuboreshwa. Ndiyo utaratibu wa sheria zote
duniani.”
“Sasa anapofika mahali anayeleta wazo ni Rais, lakini kwa
bahati mbaya anayekwenda kupindua pia ni Rais na amekwenda mbali zaidi kiasi
cha kusema kwamba kama Serikali tatu ile ile ambayo yeye ameisaini itapatikana,
jeshi litapindua nchi.
“Anayezungumza ni Rais, hakuna mamlaka nyingine inayoweza
kutengua kitendawili hiki. Wanaweza kuja maaskofu, ...masheikh, asasi
mbalimbali... hatimaye hakuna anayeweza kutengua kwa sababu aliyeufanya ni
mwenye mamlaka ya juu,”alisema.
Dk Slaa aliyewahi kuwa Mbunge wa Karatu kwa vipindi tofauti
alitaja mambo matano anayopaswa kuyafanya Rais Kikwete ili wajunge wa Bunge
Maalumu la Katiba wanaounda Ukawa waweze kurejea bungeni.Aliainisha la kwanza
ni majadiliano kuwa na misingi iliyo wazi akisema Ukawa haipo tayari kufanya
mambo na kuishia kupewa pipi na kwamba Katiba Mpya lazima ipatikane kwa
maridhiano.
Alitaja jambo la pili kuwa ni lazima wao , Ukawa
wahakikishiwe kuwa kanuni hazichezewi baada ya kupitishwa na siyo kama
ilivyofanya CCM, baada ya Ukawa kutoka bungeni akisema hatua hiyo ni sawa na
uhuni. Lingine ni kuhakikishiwa kitakachojadiliwa ni rasimu iliyowasilishwa na
Tume ya Marekebisho ya Katiba si kingine.
Huku akitoa mfano wa hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere ya
Juni, 1965 akisema ndiyo iliyowajibu CCM kuhusu msimamo wa Serikali mbili
waliodai ni kuenzi aliyoanzisha Nyerere, Dk Slaa alisema;
“Itakuwa upumbavu kama watu wataamini kwamba katiba
haibadiliki, hata kama imedhihirika kuwa haitoshelezi tena haja ya wananchi kwa
wakati ule.”
Alihoji kwamba ikiwa Mwalimu Nyerere alitoa kauli hiyo
kipindi hicho ni nini msingi wa CCM kuendelea kung’ang’ania hoja zao wakidai
kudumisha misingi yake (Nyerere). Alifafanua kuwa kimsingi katiba hubadilishwa
kwa haja mbalimbali za wananchi akitaja baadhi yake kuwa ni za kijamii,
kiuchumi, kifedha.
“Kikwete ndiye mwenye rungu la Katiba Mpya, achukue nafasi
yake kama mkuu wa nchi na siyo kama mwenyekiti wa CCM...Rais wa nchi hapaswi
kuwagawa Watanzania na wala hatakiwi kuonyesha tofauti kama alivyofanya yeye
alipozindua Bunge,” alisema.
Aliongeza: “Arudishe mchakato katika reli, aite wadau
wakiwamo Ukawa na asipofanya hivyo msimamo wetu ni ule ule wa kusimamia na
kutetea maoni ya wananchi waliyoyatoa.”
akuna haraka ya Katiba
Hata hivyo, Dk Slaa alisema kuwa hakuna haja ya kukimbizana
kupata Katiba Mpya kwa kutaka kulazimisha iweze kutumika katika uchaguzi mkuu
ujao mwakani, akihadharisha kuwa hilo likifanyika haitapatikana katiba bora.
Alisema kuwa awali, Rais Kikwete aliwatangazia Watanzania
kwamba Katiba Mpya ingepatikana Aprili 26 mwaka huu katika maadhimisho ya miaka
50 ya Muungano, lakini ameshindwa kutimiza ahadi hiyo.
“Hata kama ikipatikana (Katiba) Machi au Aprili mwakani, bado
haiwezi kutumika katika uchaguzi huo kwani kutakuwa na utaratibu wa kufumua
sheria zote hizo ili zifanye kazi kama Katiba inavyoelekeza, jambo ambalo
haliwezi kutekelezwa kwa kipindi kifupi,” alisema.
Alisema kuwa kinachotakiwa sasa ni Bunge kufanya marekebisho
ya katiba iliyopo ya mwaka 1977 katika vipengele viwili ili kuhakikisha
uchaguzi huo unafanyika ukiwa huru na haki.
Alivitaja vipengele hivyo kuwa ni suala la kuwapo kwa Tume
Huru ya Uchaguzi na rais kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 52 ya idadi ya
wapigakura.
“Huwezi kuongoza taifa ambalo hukuvuka asilimia 50 ya kura
zote, mfano mwaka 2010 Kikwete waliomchagua hawafiki robo ya waliopiga kura,
sasa, jambo hili linahitaji kufanyiwa marekebisho,” alisema.
Aliongeza: “Rais anaweza kuwa na dhamira nzuri, lakini kuna
wanachama ndani ya CCM ambao hawapendi katiba ipatikane katika kipindi cha
uongozi wa Rais Kikwete na yeye hafanyi uamuzi wake bali husukumwa na
wanaomzunguka, wanaotamani utawala.”
Atahadharisha viongozi wa dini
Kuhusu viongozi wa dini kuwataka Ukawa unaoundwa na vyama
vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kurejea bungeni, katibu mkuu huyo wa Chadema
alisema, maaskofu wanatakiwa kuwa makini kabla ya kutoa kauli hizo.
Alisema kilichowatoa Ukawa bungeni ni kutokufuatwa kwa
misingi ya mjadala wa katiba na maoni ya wananchi kudharaulika na kuanza
kujadiliwa kwa Rasimu ya CCM.
“Maaskofu wangu hawajui kilichomo bungeni, hoja yetu ni je,
tunarudi tutajadili rasimu iliyopo mezani? Hatuwezi kukubali kuona rasimu
ikichakachuliwa.
“Viongozi wangu wa dini nawapenda sana, ila nawasihi
wasiingie katika hili kwani litakuja kuwahukumu siku ya mwisho kwa kutoa kauli
ambazo hawajafanyia utafiti,”alisema.
Aliongeza: “Wakumbuke, katika Biblia kuna maandiko yanasema;
yeyote anayewapotosha wadogo, anastahili kufungiwa jiwe shingoni. Wabunge
wanapotoka bungeni wanajali wakitaka sauti ya wanyonge isikike, waliotutuma
wanataka haki itendeke.
“Ukawa inapinga ‘dictatorship of the majority’(Udikteta wa
wengi). Tunachofanya ni njia halali ya mapambano inayoweza kutumika dunia nzima,
pale wengi wanapogeuka madikteta.”
Julai Mosi, Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania
(TEC), liliwataka Ukawa kurudi bungeni bila masharti na kuendelea na mjadala wa
Katiba Mpya kwa manufaa ya taifa.
Pia, Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG),
Jimbo la Mashariki Kaskazini, Geoffrey Massawe aliomba wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba kuungana na kuwa kitu kimoja katika mchakato huo wa Katiba.
Askofu Massawe alitoa ombi hilo wakati wa ibada maalumu ya
sherehe ya maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo nchini
iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kinondoni, Dar es Salaam.
Akitoa salamu za TEC wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya
uaskofu wa Tarcisius Ngalalekumtwa kwenye Uwanja wa Kichangani, Iringa, Makamu
Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi alisema ni vyema wajumbe hao wakarudi
kwenye bunge hilo linalotarajia kuanza Agosti 5, mwaka huu.
“Ninatumia neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee bungeni
mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au kufanya mizengwe mingine na kutupatia Katiba
Mpya isiyotufaa, nitawaomba Watanzania wote tuweke uzalendo mbele na kuikataa
rasimu ya Katiba itakayoletwa pia tuwanyime uongozi katika uchaguzi mkuu ujao,”
alisema.
Nguvu ya Chadema
Katibu Mkuu huyo alisema chama hicho hivi sasa kina nguvu
nchi nzima kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu hivyo kinaweza kupambana vyema na
CCM.
Alisema wamekuwa wakitumia ruzuku wanayoipata kutoka
serikalini ya Sh233 milioni kila mwezi kupeleka vitendea kazi katika majimbo na
kanda.
“Tuliamua kufanya hivyo kwani tulivyokuwa tukipeleka fedha
walikuwa wakizigombania na mpaka sasa kanda kumi zina gari moja moja na
wilayani kuna pikipiki moja pamoja na kompyuta.
“Yaani, sasa hivi kama CCM ina wachezaji 11 uwanjani nasi
(Chadema) tunao wachezaji 11 ni tofauti na ilivyokuwa mwanzo hivyo mpira
unachezeka sawasawa,” alisema.
Aliongeza kuwa kanda na majimbo yanajiendesha kwani
wamepeleka zaidi ya kadi milioni 75 ambazo kila kadi ni Sh1500 na ada ni
Sh1,000 hivyo fedha hizo zinaweza kuendesha ofisi hizo bila kutegemea fedha
kutoka makao makuu.
Ofisi ya Zitto
Akizungumzia kubadilishwa kwa matumizi kwa ofisi ya
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Dk Slaa alisema amefanya hivyo
kutokana na mhusika kutoitumia kwa muda mrefu.
“Nimefanya hivyo kwani siwezi kuiacha ofisi ikakaa bila mtu
wakati kuna watu wangu hapa wanabanana na hata mkipita mtaona nimebadili
matumizi ya ofisi,” alisema Dk Slaa.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment