Baraza la Madaktari Tanganyika (TMC) limesema linasubiri
majibu ya ripoti zilizoundwa kuchunguza sakata la utupaji holela wa viungo vya
binadamu, kabla ya kutoa adhabu stahiki
kwa madaktari waliohusika.
Msajili wa baraza hilo, Peter Luena alisema ingawa ofisi yake haina mamlaka ya
kukichukulia hatua za kinidhamu Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na
Teknolojia
(IMTU) kinachodaiwa kutupa viungo hivyo, inao uwezo wa kutoa adhabu za aina nne
kwa madaktari watakaobainika kuhusika.
Wiki iliyopita Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Jeshi la
Polisi waliunda timu mbili tofauti kuchunguza namna ambavyo viungo vya binadamu
kutoka IMTU vilivyotupwa katika Bonde la Mto Mpiji, jijini Dar es Salaam.
Luena alisema maadili ya udaktari yanaeleza kuwa iwapo
daktari amekiuka taratibu za kazi ataitwa mbele ya Baraza la Madaktari na
kusomewa mashtaka yake.
“Iwapo atapatikana na kosa, sheria yetu ina hatua nne za
adhabu; onyo la kawaida, karipio kali, kusimamisha usajili wa daktari husika na
kama ni kosa kubwa anafutiwa usajili kabisa,” alisema.
Hata hivyo, alisema daktari atakayepewa adhabu anaweza
kujitetea na kuomba apunguziwe adhabu husika, akikataliwa anaweza kukata rufaa
Mahakama Kuu ya Tanzania.


No comments:
Post a Comment