Kumetokea shambulizi katika shule moja ya upili wakati
wanafunzi wakiwa wamekusanyika shuleni humo mjini Potiskum Kaskazini Mashariki
mwa Nigeria.
Hata hivyo hakuna taarifa kamili kuhusu idadi ya majeruhi
kufikia sasa ingawa duru zinasema kuwa wanafunzi kadhaa wameuawa na wengine
wengi kujeruhiwa.
Shambulizi lilitokea wakati wanafunzi wakiwa wamekusanyika
wakati wa asubuhi. Mji wa Potiskum ambapo shule hiyo ipo, umekuwa kitovu cha
mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanywa na Boko Haram.
Shule hiyo ni ya mafunzo ya sayansi. Mwalimu mmoja
alinukuliwa akisema kuwa alisikia mlio mkubwa wa kutisha wakati bomu hilo
lilipolipuka.
Kundi la wapiganaji wa kiisilamu Boko Haram huenda ndilo
limefanya shambulizi hilo, ila taarifa bado hazijathibitisha hilo.
Kadhalika kundi hilo limekuwa likishambulia shule katika
harakati zake za miaka 5 likitaka kuunda dola ya kiisilamu huku likipinga elimu
ya kimagharibi.
Wiki jana shambulizi la kujitoa mhanga lilifanyika mjini
humo na kuwaua watu 15 wakati wa maandamano ya kidini.
No comments:
Post a Comment