Magari yenye namba za
usajili wa Tanzania zimepigwa marufuku na uongozi wa uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya na kusababaisha adha kwa mamia ya
watalii na Watanzania wengine ambao wanafika katika uwanja huo kuchukua wageni.
Amri hiyo ilitolewa tangu Desemba 22, mwaka jana baada ya
askari wanaokagua magari yanayoingia
uwanjani hapo kuanza kuzuia magari yote
kutoka Tanzania kuingia wakidai kuwa wameagizwa na viongozi wao kufanya
hivyo.
Wakizungumza na gazeti hili katika eneo la Astro lilipo geti
la kwanza la kuingia uwanjani hapa, madereva wanaowapeleka watalii katika
uwanja huo kutoka kampuni mbalimbali za kitalii, walisema hatua hiyo imewapa
adha kubwa wageni hasa watalii ambao wengi walishangazwa kuzuiwa kuiingia
katika uwanja huo wakiwa katika magari yanayotokaTanzania.
Ruben Kiondo, dereva wa kampuni ya Rainbow Shuttle. alisema
anashangazwa na usumbufu wanaoendelea kupata hasa watalii wanaokuja nchini Tanzania huku
serikali ikikaa kimya.
“Huwezi kuamini lugha
isiyo nzuri wanayojibiwa watalii wanaoelekea Tanzania kupitia uwanja huu wakihoji askari wanaozuia magari ya Tanzania
kuingia uwanjani, mara wanaambiwa kwanini msipande ndege huko uwanja wa
Kilimanjaro, tutawazuia msipite hata
mpaka wa Namanga,” alisema Kiondo.
Mfanyabiashara kutoka Arusha ambaye naye alifika katika
lango la kuingilia uwaanjani hapoa juzi akiwa na gari dogo lenye namba za
usajili za Tanzania, Patel Bhatia, alisema alifika katika uwanja huo kwa lengo
la kuwachukua ndugu zake kutoka Uingereza, lakini alizuiwa kuingia na kukaa nje hadi alipowasiliana na
ndugu ambao walichukua teksi kumfuata
nje ya uzio wa uwanja huo.
Mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji ya River Side
inayobeba watalii wa ndani na nje, Moses
Kingori, alisema hatua hiyo imewaathiri kwa kiwango kikubwa kibiashara na
kuleta hofu kubwa kwa watalii kutoaka Ulaya na Marekani.
“Habari hizi sasa zimeenea hasa katika sekta ya utalii,
wageni wanaogopa sana, kitendo kinachofanywa
hakijawahi kushuhudiwa, wageni wanacheleweshwa kufika kwa wakati ndani
ya uwanja tayari kupanda ndege hili ni jambo baya sana,” alisema Moses.
Mkurugenzi wa kampuni ya Rainbow, Mathew Mollel, alisema
wageni wanaotumia magari ya kampuni yake
wamepata usumbufu mkubwa sana toka zoezi hilo lianze.
Akizungumzia kuhusu hali hiyo, Waziri wa Wizara ya
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema hana taarifa rasmi za
tukio hilo na kulaumu watendaji wa ngazi za chini katika serikali ya Kenya kwa
kufanya vitendo vinavyotishia uhai wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
“Ni vitendo ambavyo havikubaliki, sio sawa kabisa na
vitaiangamiza Jumuiya ya Afrika Mashariki, hatukubali hata kidogo, kuna mengi
yanayotokea huko dhidi ya maslahi ya
Tanzania na kwa kweli vinaweza kuiua jumuiya,” alisema Sitta.
Alisema kuwa serikali ya Tanzania itachukua hatua haraka
kufuatilia jambo hilo .
“Mimi na waziri mwenzangu wa jumuia upande wa Kenya
tunatambua msimamo wa Rais wa Kenya kuhusu jumuia, lakini nina mashaka na
watendendaji wa chini katika serikali na mamlaka kadhaa za Kenya zinaweza
kuleta matatizo makubwa katika muungano wetu,” alisema Sitta.
No comments:
Post a Comment