Mkurugenzi
wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama,
ametamka kuwa yeye si Meneja wa malkia wa nyimbo za injili nchini, Rose
Muhando akisema amekuwa akishirikiana naye katika mazingira ya kawaida
kama ilivyo kwa waimbaji wengine.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Msama kwa vyombo vya habari juzi, yeye akiwa mlezi
wa waimbaji wote wa muziki wa Injili, amekuwa akishirikana nao kwa
karibu kutokana na nafasi yake katika huduma hiyo ya uimbaji kwa kipindi
cha miaka 15.
Msama,
mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya muziki wa injili nchini
kutokana na kuandaa matukio ya muziki huo kama Tamasha la Pasaka,
uzinduzi wa albamu na Tamasha la Krismas, alisema ameamua kutoa tamko
hilo kutokana na malalamiko ya muda mrefu ambayo amekuwa akipata juu ya
Rose.
“Nimekuwa
nikipokea malalamiko mengi ikiwemo kutoka kwa viongozi wa kiroho
wakiwemo wachungaji, kwamba pengine nimekuwa nikimzua Rose (Muhando)
katika mtamasha wanayomualika na kushindwa kutokea.
“Lakini,
naomba watumishi wa Mungu wanielewe katika hili, sipokei mialiko wala
simzuii Rose. Mimi ninapokuwa na matamasha, nimekuwa nikimualika kama
wafanyavyo wengine.
“Nimekuwa nikimlipa kiasi cha fedha anachotaka na hakuna zaidi, hivyo mimi sio Meneja wake,” alisema Msama katika taarifa hiyo na kuongeza:
“Agosti
mwaka huu, kampuni yangu ilidhamini uzinduzi wa albamu yake ya Kamata
Pindo la Yesu, haikuwa na maana kwamba ni Meneja wake.
“Nilimualika
uzinduzi wa albamu ya Uko Hapa ya msanii John Lissu Oktoba mwaka huu,
nilimlipa fedha, lakini hakutokea kama ambavyo amekuwa akifanya kwa
wengine ambao wamekuwa wakilalamikia tabia hiyo,” alisema Msama.
“Pia wiki iliyopita nilikuwa na Tamasha la Krismasi tulikubaliana aje katika maonesho hayo, lakini hakutokea na tulishamlipa,”alisema Msama kwa masikitiko na kuongeza kuwa amemsamehe na anamuombea kwa Mungu aweze kubadilika.
Alieleza
kuwa hana tatizo na mwimbaji huyo, wala hana ugomvi naye, lakini
amekuwa akipata taabu kutoka kwa baadhi ya wachungaji pale Rose
anapoalikwa halafu hatokei na inaonekana yeye ndiye amemzuia.
“Sijawahi kupokea mialiko kwa niaba ya Rose, kila kitu anafanya mwenyewe, hivyo ni vyema wadau wakafahamu hilo,” alisema Msama na kusema angekuwa mwepesi wa kulalamika, angeshafanya hivyo muda mrefu dhidi ya Rose.
Aidha,
Msama amekana kuhusiana na madai ya Rose kutumia dawa za kulevya na
kusisitiza kuwa hajawahi kumuona akijidunga kama ambavyo baadhi ya
vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti na kuongeza kama ikiwa ni kweli,
hilo pia ni suala binafsi.
“Baadhi
ya vyombo vya habari vinaandika ni mjamzito, nafikiri pia hayo ni mambo
yake binafsi na hakuna mtu mwenye haki au uhalali wa kuhoji hilo.Yule
ni mtu mzima na mwenye kujielewa,” alisema Msama.
Rose
ni mwimbaji mahiri wa muziki wa injili nchini aliyejipatia sifa ndani
na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki ambaye mwishoni mwa mwaka 2013,
alisaini mkatabawa kufanya kazi na kampuni ya muziki ya Sony ya Afrika
Kusini.
Miongoni
mwa albamu zilizompa umaarufu Rose kiasi cha kuwa alama ya mafanikio ya
muziki wa injili nchini, ni ‘Uwe Macho,’ Nyota ya Ajabu (Zawadi ya
Krismasi), Jipange Sawasawa, Kitimutimu, ‘Mungu Anacheka’ na Wololo na
Kamata Pindo la Yesu aliyoachia hivyo karibuni.
No comments:
Post a Comment