Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, April 8, 2015

Kisiwa Zanzibar hatarini kutoweka

Kisiwa cha Mnemba


JUHUDI za haraka zinahitajika kuchukuliwa ili kukihami kisiwa kidogo cha Mnemba kilichopo Matemwe mkoa wa Kaskazini Unguja, kutokana na kasi ya maji kuvamia maeneo ya nchi kavu, kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mjumbe wa Kamati ya Kulinda Mazingira mkoa wa Kaskazini Unguja, Makame Mussa Makame alisema hayo wakati alipozungumza na gazeti hili kuhusu athari za mazingira zinazoikabili kisiwa hicho na mikakati ya kukihami na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
 
Alisema maji ya baharini, yamekuwa yakipanda juu na kuingia maeneo ya fukwe, karibu na majengo ya hoteli ya kitalii iliyopo katika kisiwa hicho na hivyo kutishia maendeleo ya sekta ya utalii.
“Juhudi za haraka zinahitajika kwa Serikali kuweza kukihami kisiwa cha Mnemba ambacho kipo katika hatari ya kutoweka kutokana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ya maji ya bahari kuja juu kwa kasi na kuharibu mazingira,” alisema.
Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar, Sheha Mjaja alikiri kuwepo kwa hatari za kisiwa cha Mnemba, kuvamiwa na kasi ya maji yanayotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mjaja alisema athari kama hizo, zipo kwa baadhi ya visiwa vilivyopo Unguja na Pemba ambavyo vinakabiliwa na kasi ya maji kuvamia maeneo ya makaazi ya watu.
Visiwa vidogo ambavyo vinatajwa vipo katika hatari ya kuathirika na mabadiliko hayo ya tabia ya nchi ni Mtambwe Mkuu, Kisiwa Panza na Kokota, ambapo baadhi ya wananchi wameanza kuhama na kuja nchi kavu.
Mjaja alitaja baadhi ya juhudi zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo kuwa ni kupanda miti ya aina mbalimbali, ikiwemo mikoko pembezoni mwa fukwe za bahari ili kudhibiti hatari hiyo.
“Athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, zimeleta majanga makubwa, ikiwemo kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya nchi kavu na kutishia maisha ya wananchi wanaoishi maeneo hayo,” alisema.
Alisema tayari zaidi ya mikoko 60,000 imeoteshwa na kusambazwa kwa wananchi mbalimbali kupitia vikundi vya ushirika kwa ajili ya kukabiliana na hatari ya majanga hayo.
Mikoko ni miti maarufu inayoota pembezoni mwa baharini, ambayo husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia nguvu ya kasi ya maji kuvamia maeneo ya ardhi na kusababisha uharibifu mkubwa.

No comments:

Post a Comment