Baadhi ya wakazi wa kisiwa cha Mafia, mkoani Pwani, wamehoji kuhusu
kutoonekana kwa boti kubwa na ya kisasa iliyoonyeshwa ikizinduliwa na
Rais Jakaya Kikwete, mwaka juzi wakati akizindua gati jipya wilayani
humo.
Wakati wa uzinduzi huo wananchi walionyeshwa boti hiyo ya kisasa
ambayo waliambiwa ingetumika lakini tangu wakati huo haijaonekana na
watu wanendelea kutumia boti zisizo salama.
“Tulipoona boti mpya tukajua tatizo la usafiri limekwisha lakini
mara baada ya uzinduzi wa gati hiyo boti hatukuiona tena hadi leo,
tunaendelea kuhangaika na usafiri ambao si salama”, alisema Jumanne
Mwinyimvua
Kukosekana usafiri wa uhakika na salama wananchi wa kisiwa hicho
wamedai maisha yao yako hatari kwa kukosa usafiri wa uhakika licha ya
juhudi zilizofanywa za kujenga gati ambayo haitumiki.
Wamedai wamekuwa wakitumia mitumbwi na boti ndogo ambazo mara nyingi si salama na wakati mwingine huzimika katikati ya maji.
“Kutokana na ugumu wa usafiri watu wamekuwa wakifa mara kadhaa
baada ya boti kupinduka au kuzimika katikakati ya maji na hatuna
mbadala huo ndio usafiri, wakati mwingine uko na familia yake unaomba
mungu ufike salama tu maana hakuna jinsi”, alisema Mwajuma Mohamed
mkazi wa Mafia.
Mkazi mwingine wa kisiwa hicho Hussen Omar alisema wanaiomba
serikali kufanya jitihada za lazima katika kuhakikisha inaimarisha
usafiri katika kisiwa hicho na kuwa viongozi hawaoni kero hiyo kwa kuwa
wakienda Mafia hutumia usafiri wa ndege.
Mbali ya ukosefu wa usafiri wa uhakika pia wakazi wa visiwa vidogo
vilivyopo ndani ya kisiwa cha Mafia vya Chole, Jibondo, Bwejue na Juani
wanakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama kwani maji yaliyoko
katika visiwa hivyo ni ya chumvi na kuwalazimu kununua maji kutoka
kisiwa kikubwa cha Mafia kwa gharama ya Sh. 1000, kiasi ambacho hawawezi
kumudu.
"Usafiri wa kupeleka maji kwenye visiwa hivyo ni wa kukodi mtumbwi
au boti kwa gharama ya Sh. 150,000 na wauzaji huuza kwa Sh. 1,000 kwa
ndoo moja ya lita 20," alisema mmoja wa wakazi wa Mafia Clever
Mwaikambo.
Uchunguzi wa NIPASHE ulibaini kuwa wafanyabiashara wanashindwa
kupeleka vyombo vyao vya usafiri kutokana na kukosekana kwa gati upande
wa pili wa Nyamisati ambapo boti hunasa kwenye mchanga na hivyo
kuharibika na kufanyia matengenezo ya mara kwa mara
No comments:
Post a Comment