Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 27, 2015

KAULI ya Mgombea Julias Mtatiro Baada ya Kushindwa Ubunge Segerea Yawagusa Wengi..Adai Kilichotokea Kiwe Funzo Kwa UKAWA


HATUWEZI KUSHINDA UBUNGE SEGEREA...
Ndugu zangu, kwa moyo mkunjufu kabisa napenda kuwajulisha kuwa hatuwezi tena kushinda ubunge wa jimbo hili kwenye uchaguzi uliofanyika jana.
Matokeo ya majumuisho ya kila kata yanaonesha kuwa mgombea wa Chadema, Bi. Anatropia Theonest ana wastani wa kura 2000 - 2500 kwa kila kata.
Mimi nina wastani wa kura 4000 - 5000 kwa kata na mgombea wa CCM ana wastani wa kura 5000 hadi 6000 kwa kata.
Hii ina maana kuwa kura za UKAWA kama zingelipigwa kwa mgombea halisi wa UKAWA tungeishinda CCM kwa zaidi ya kura 20,000 lakini kwa sababu zimepigwa kwenda vyama viwili tunaweza kushindwa kwa wastani wa kura 5000 hadi 10,000.
Haya yaliyotokea hapa Segerea ni funzo kubwa kwa vyama vyetu na wanasiasa wetu kuheshimu na kusimamia

 
 makubaliano, kuwa na roho ya kufikiria mustakabali wa taasisi na watu wetu kuliko MASLAHI BINAFSI. Kwa hatua ya sasa sitaeleza hujuma za ndani kwa ndani tulizofanyiana ndani ya UKAWA hadi kufika hapa.
Nachoweza kusema ni Asante Mungu na asante wana Segerea, asante watu wote waliojitoa kufa na kupona kutusaidia, lakini pia asante kwa wale wote waliotusaliti kimya kimya ili kuchochea mgawanyiko wa kura hizi.
Naahidi kushiriki katika hatua zote za kumsaidia mshindi wa uchaguzi wetu ili atangazwe rasmi kuwa mbunge wa wana Segerea. Mimi nitaendelea na majukumu mengine lukuki ya kulijenga taifa letu.
Kwa sababu yaliyosababisha kukosa ushindi wetu ni mambo ya ndani ya vyama vyetu, sitachukua hatua zozote wala kukata rufaa kwa sababu wananchi hawakutunyima ushindi, tumeugawanya wenyewe.
Nawapongeza madiwani wa UKAWA walioshinda kwenye kata zote 13 za jimbo letu, tulishirikiana na kupambana pamoja hadi kuleta ushindi huu, nawataka wachape kazi kufa na kupona na waisimamie manispaa ya Ilala bila woga, nawaomba wakatumie mipango na ushauri tuliowahi kupanga pamoja ili kuwatendea wana Segerea yale waliyoyatarajia.
Mwisho, nataka kuwaeleza watanzania wote kuwa sina kinyongo na mtu yeyote kwa matokeo haya. Mimi ni kati ya watu wanaoamini kuwa SIASA SI AJIRA...Nitaendelea kuwatumikia watanzania kwa njia zote muhimu nje ya vyombo vya maamuzi.
Nataka kuwaambia wananchi wa Segerea kwamba niko imara sana, sijayumba wala kutetereka, nawapenda sana nyote na poleni na MSHTUKO wa matokeo haya na muda si mrefu tutayaweka hapa.
Ni mimi,
Mtatiro Julius,
Segerea.

No comments:

Post a Comment