Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, December 19, 2015

RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI AJALI YA BASI LA NEW FORCE IRINGA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza kufuatia ajali ya basi la kampuni ya New Force kugongana na lori, na kusababisha vifo vya watu 12, na wengine 15 kulazwa Hospitali.
Ajali hiyo imetokea tarehe 18 Desemba, 2015 Majira ya saa nane mchana katika Kijiji cha Mahenge, Wilaya ya Kilolo Mkoani IRINGA ambapo Basi la kampuni ya New Force lenye namba T 483 CTF lililokuwa limebeba abiria 49 limegongana na Lori la Kampuni ya Reign-ford Limited lenye namba T 616 BEF na Tela lake lenye namba T 320 DEF lililokuwa na shehena ya mbao .
Rais Magufuli amemuomba Mkuu huyo wa mkoa kufikisha salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote 

 
ambao wamepoteza ndugu zao katika ajali hiyo mbaya"Nimesikitishwa sana na kutokea kwa ajali hii, ninawapa pole nyingi wote waliopoteza ndugu zao na ninawaombea Majeruhi wote wapone haraka ili waungane na familia zao na kuendelea na shughuli zao za maendeleo" amesema Rais Magufuli.
Amewaombea marehemu wote kwa Mwenyezi Mungu ili azipumzishe roho zao mahali pema peponi, Amina.Aidha Dkt. Magufuli ametoa wito kwa watuaji wote wa barabara hususani madereva kuwa waangalifu waendeshapo vyombo vya usafiri na amewakumbusha wananchi wanaotumia barabara kwa kusafiri ama kusafirisha mizigo kutoa ushirikiano kwa vyombo husika pale wanapobaini kuwepo vitendo ambavyo ni chanzo cha ajali.

Imetolewa na;  Gerson Msigwa,
                        Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
                        18 Desemba, 2015

No comments:

Post a Comment