Kama wewe ni msanii, huenda mwaka huu ukaanza kukosa show au
kutajwa kwenye tuzo kama hujaenda kujisajili kwenye Baraza la Sanaa la Taifa,
BASATA.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote
nchini kuhakikisha wamesajiliwa na kuwa na vibali vya Baraza kwani kufanya
vinginevyo ni kuvunja sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 iliyolianzisha
BASATA ambayo inamtaka mtu yeyote anayejihusisha na shughuli za Sanaa kuwa
amesajiliwa na kupewa kibali na BASATA.
Aidha, BASATA linawaagiza Wakuzaji Sanaa wote (Mapromota)
wanaoendesha matukio ya Sanaa kama vile matamasha, mashindano, maonyesho na
utoaji tuzo nchini kuhakikisha wanafanya kazi na Wasanii waliosajiliwa na wenye
vibali vya BASATA na si vinginevyo.
Sambamba na hili, BASATA linawaagiza wamiliki wote wa studio
(Production Houses) zinazozalisha kazi za Sanaa kuzisajili mara moja na
kuhakikisha zinakuwa na vibali halali vya Baraza la Sanaa la Taifa.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa sheria hii ya BASATA, Baraza
limepewa mamlaka ya kutoa vibali na kuratibu matukio yote ya Sanaa nchini hivyo
kuanzia sasa Baraza litaanza udhibiti wa matukio haya ya Sanaa hasa katika
kuongeza sharti la kuwataka waandaaji wote wa matukio ya Sanaa kuwataka wasanii
watakaoshiriki matukio yao kuwa wamesajiliwa na kupewa vibali na BASATA.
BASATA halitavumilia kwa namna yoyote kuona Mkuzaji Sanaa
(Promota) akitumia wasanii wasiosajiliwa na kuwa na vibali kutoka BASATA kwani
kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi hasa sheria hiyo namba 23 ya mwaka 1984
inayoelekeza usajili na utoaji vibali kwa wadau wote wa Sanaa.
Itakumbukwa kwamba mnamo Mwaka 2013 Serikali kupitia Sheria
ya Ushuru wa Forodha ilitangaza rasmi kuzirasmisha sekta za muziki na filamu.
Sheria hii pia inawataka wasanii wote nchini kusajiliwa na kupewa vibali na
BASATA na kinyume chake ni uvunjaji wa sheria.
Hata hivyo, toka kuanza kwa mchakato huu wa urasmishaji
sekta ya Sanaa ni wasanii wa muziki wa injili pekee ndiyo wamekuwa wakisajiliwa
kwa wingi huku wale wa muziki wa kizazi kipya na filamu wakisuasua bila kuwepo
kwa sababu za msingi.
BASATA limekuwa likichukua hatua kadhaa kurahisisha mfumo wa
usajili wa wasanii ambapo kwa sasa msanii anaweza kupata fomu ya usajili
kupitia mtandaoni www.basata.go.tz au kwa maafisa Utamaduni wa Wilaya na
baadaye kujaza fomu na kutakiwa kuziwasilisha BASATA zikiwa zimeambatanishwa na
wasifu binafsi (CV) wa Msanii husika.
Aidha, gharama za usajili ni kiasi cha Tsh. 75,000/- pekee
ambapo fomu hupatikana kwa Tsh. 5, 000/-, Usajili 30,000/- na kibali cha kila
mwaka 40,000/-
Kwa upande wa studio na wakuzaji Sanaa (Mapromota) gharama
ni sawa na za msanii isipokuwa tofauti huwa kwenye kibali abapo wao hulipa
kiasi cha Tsh. 200.000/- kwa mwaka.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
No comments:
Post a Comment