Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, March 11, 2016

ZAIDI YA WASICHANA 500 JIJINI MWANZA WANUFAIKA NA MRADI WA BINTI BOX.‏

Wasichana wa Shule ya Sekondari Luchelele wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji toka DidaVitengeWear Foundation mara baada ya kupokea taulo za usafi (Pedi) na Elimu ya Usafi wa mwili na uzazi chini ya mradi wa Binti Box unaotekelezwa katika shule za Sekondari na Msingi kanda ya Ziwa.
Katika kusheherekea siku ya Wanawake Duniani Machi 08,2016, taasisi ya kusaidia wanawake na wasichana yenye makao makuu jijini Mwanza, DidaVitengeWear Foundation, Imefanikisha kugawa taulo za usafi zaidi ya 2,000 kwa wasichana zaidi ya 600 wa shule ya msingi Igombe na Shule ya Sekondari ya Luchelele zote za Jijini Mwanza kupitia mradi wa kuwasaidia Mabinti kufikia malengo yao, ujulikanao kama ‘Binti Box’.  

Hatua hiyo pia imefikiwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya taasisi hiyo pamoja na Mtandao wa Wanawake jijini Mwanza wa ‘Women Roundtable’, na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM) Mh.Stanslaus Mabula, Mbunge Viti Maalum Wanawake Mkoani Mwanza Zawadi Kiteto na Mbunge wa Viti Maalum Vijana Mkoani Mwanza Mh.Maria Kangoye Ndila 


Binti Box ni mradi ulioanzishwa kwa lengo la kuwasaidia watoto wa kike waliopevuka kubaki shule na kuimarisha mahudhuria ya wasichana shuleni kwa kuwapatia vifaa vya usafi vitakavyowasaidia wakati wa siku zao za hedhi. Wasichana wengi hasa wa vijijini hukosa kwenda shule kwa siku 5 mpaka 7 kwa mwezi kwa sababu ya kukosa vifaa vya usafi wakati wa mzunguko wa hedhi, hivyo mradi huu kwa upande wa kanda ya ziwa ni mkombozi kwa mabinti wengi kuhudhuria shule na kuinua kiwango cha ufaulu katika masomo yao.

Akiongea wakati wa kugawa taulo hizo za usafi mashuleni, Bi. Khadija Liganga, Mratibu wa Mradi na Mkurugenzi wa DidaVitengeWear Foundation, alieleza kwamba, elimu ya wasichana ni jambo la msingi katika jitihada za kuleta maendeleo kwa nchi masikini kwa sababu mafaniko ya wanawake hasa katika elimu inamaanika kuwa na faida ya muda mrefu na huenda mbali Zaidi katika kuinua uchumi wa jamii na nchi.

“Kuna sababu nyingi zinazochangia kudumaa kwa ustawi wa elimu ya mtoto wa kike hasa wale wa vijijini, tatizo la ukosefu wa vifaa vya usafi kwa mabinti wakati wa hedhi kwa kila mwezi nayo imeibuka kuwa ni tatizo sugu linalofumbiwa macho na wadau wengi wa maendeleo katika nchi zinazoendelea na Tanzania ikiwemo. Wasichana hawa hujawa na uwoga na kuhofia kupoteza thamani yao na utu wao wawapo shuleni au mbele za watu na kuwafanya wasihudhurie darasani au kutokwenda shule na matokeo yake wengi huacha shule,” amesema Bi. Khadija Liganga  

Bi.Khadija aliendelea kusema kwamba “Baada ya kutembelea baadhi ya shule zilizo pembezoni na miji tumegundua tatizo ni kubwa, tukapata uwelewa wa kutosha na tukaona ni vyema badala ya kuandaa makongamano ya wanawake wakati wa sherehe za Siku ya Wanawake Dunaini 2016, kwanini tusiguse eneo ambalo ndio chimbuko la ukandamizaji wa maendeleo ya Mwanamke, ambalo ni Elimu. Ndipo tukaja na huu mradi utakaokuwa endelevu wa ‘Binti Box’ kwa lengo la kutoa taulo za usafi kwa mabinti wa shule za msingi na sekondari pamoja na elimu ya usafi wakati wa siku za hedhi”

“Tungependa kuwashukuru watu wote pamoja na taasisi mbalimbali kwa mchango wa o wa maboksi ya taulo za usafi. Huu ni mwanzo tu, huku mipango ikiwa ni kuongeza uwezo wa mradi kuweza kutoa huduma hii kwa shule za sekondari na msingi katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, tuko tayari kushirikiana na watu binafsi au taasisi yoyote katika kumkomboa mtoto wa kike” alisema Bi. Khadija Liganga

Lengo la Mradi wa Binti Box ni kuwapatia elimu ya uzazi,afya,kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuwapatia taulo za usafi wasichana wa sekondari na shule za msingi waliopo katika umri wa kuvunja ungo katika mikoa ya Mwanza na Mara. Mradi unatekeleza mpango wa taifa kwa vitendo wa kuhakikisha watoto wa kike hawabaki nyuma bali wanapata fursa sawa na wenzao wa kiume na kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike.
Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa DidaVitengeWear Foundation ambae pia ni Mratibu wa Mradi wa Binti Box akijadiliana jambo na Mbunge wa Viti Maalum Vijana mkoa wa Mwanza kupitia CCM, Mh. Maria Kangoye Ndila (Katikati) pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Wanawake mkoa wa Mwanza Mh. Zawadi Kiteto (Kushoto), wakati wa utekelezaji wa mradi wa kugawa taulo za usafi kwa Mabinti wa Shule ya Msingi Igombe.
Mkufunzi wa Afya ya Uzazi ambae pia ni muuguzi msaidizi kutoka kituo cha Afya cha Makongoro akitoa elimu ya usafi wa mwili na kuepuka mimba za utoto kwa wanafunzi wa kike wa shule ya msingi Igombe chini ya mradi wa Binti Box ulioandaliwa na DidaVitengeWear Foundation kwa kushirikiana na wadau mbalimbali jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment