Rais
wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, amemsimamisha kazi mmoja wa watoto
wake wa kiume kutoka ngazi ya unaibu gavana wa benki kuu ya nchi hiyo
kwa kushindwa kuorodhesha mali zake katika tume ya kuzuia rushwa nchini
humo.
Charles Sirleaf, ni miongoni mwa maafisa 46 waliosimamishwa kazi kwa kosa hilo.
Ni
mmoja wa watoto wake watatu wa kiume aliowateua kushika vyeo vya juu
kabisa baada ya kushinda muhula wa pili wa uchaguzi mwaka jana.
Wapinzani wa Bi Sirleaf wanamshutumu kwa kuendeleza upendeleo wa kindugu.
Rais
huyo amemteua mtoto wake wa kiume Fumba kuwa mkuu idara ya usalama wa
taifa, na kijana mwingine Robert kuwa mshauri mkuu na mwenyekiti wa
kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali-NOCAL.
Utawala bora
Robert
Sirleaf anayashitaki magazeti mawili nchini humo ya Independent na
Analyst, na mwanasiasa wa upinzani Jefferson Kogie kwa kumkashifu kuwa
amejinufaisha kifedha kutokana na vyeo alivyopewa.
Taarifa
kutoka ofisi ya Bi Sirleaf imesema Charles Sirleaf na maafisa wengine
45 wataendelea kuwa wamesimamishwa kazi hadi hapo watakapoorodhesha mali
zao kwa Tume ya Kuzuia Rushwa.
Maafisa
wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na mkuu wa itifaki ya rais,
David Anderson, Wakili mkuu na naibu waziri wa sheria Micah Wilkins
Wright na naibu mkurugenzi mkuu wa utangazaji Ledgerhood Rennie.
Bi
Sirleaf aliyeingia madarakani mwaka 2005 mwishoni mwa mgogoro wa vita
Uliodumu miaka 14, amekuwa akiahidi mara kwa mara kupambana na rushwa na
kustawisha utawala bora nchini Liberia.
Alitunukiwa
tuzo ya amani ya Nobel mwaka jana, muda mfupi baada ya kuchaguliwa tena
kwa muhula mwingine katika uchaguzi ulioghubikwa na tuhuma za
udanganyifu katika zoezi la upigaji kura.
Rushwa
bado inabakia kuwa kikwazo kikubwa nchini Liberia huku idadi kubwa ya
watu wakiishi katika umasikini licha ya utajiri mkubwa wa madini nchini
humo.
Mwezi
Juni taasisi ya kimataifa ya Maafa-ICG, ilitoa ripoti kutahadharisha
kuwa rushwa na upendeleo wa kindugu katika sekta mbalimbali vinaweza
kuhatarisha demokrasia nchini humo.
No comments:
Post a Comment