Uongozi
wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam umesema kuwa wakati
wowote kuanzia sasa utaihamisha stendi ya mabasi ya Mwenge na na
kuipeleka Makumbusho.
Zoezi
hilo litakwenda sambamba na kuwaondoa wamachinga wanaoendesha shughuli
zao za kibiashara katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria ikiwa ni pamoja
na pembezoni mwa barabara na ndani ya vituo vya magari.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mawasiliano wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera, wakati akizungumza na NIPASHE.
Mhowera
alisema maandalizi ya kuiondoa stendo hiyo yanaendelea na kwamba
kinachosubiriwa ni kumalizika kwa zoezi la sensa litakaloanza Agosti 26,
mwaka huu.
Aliongeza
kuwa matengenezo ya stendi hiyo mpya ya Makumbusho yanaendelea na
kwamba hadi sasa yamekamilika kwa asilimia 75 na kuongeza kuwa
kilichosababisha matengenezo hayo kuchelewa ni kuwepo kwa mgogoro kati
ya manispaa na wafanyabiashara katika eneo hilo ambao kwa sasa
umesuluhishwa.
Kwa
mujibu wa Mhowera, baada ya kukamilika kwa mabadiliko hayo, hakuna gari
litakaloruhusiwa kuingia tena ndani kwenye stendi ya Mwenge na badala
yake stendi kubwa kwa magari yote itakuwa ni Makumbusho na Mwenge
litakuwa ni eneo la kushusha na kuondoka.
Alisema
zoezi hilo litaambatana na kuwaondoa wafanyabiashara wote waliokuwa
wakiendesha shughuli zao kwenye stendi hiyo na nje kando kando ya
barabara akisema kuwa kama walivyofanya Ubungo ndivyo itakavyokuwa
kwenye eneo hilo.
Pia
aliongezakwamba wafanyabiashara wote wa bidhaa za viwandani na
mashambani wanapaswa kuendesha shughuli zao kwenye masoko
yanayotambuliwa kisheria na kwamba mikopo ipo kwa ajili ya
wafanyabiashara watakaokubali kujiorodhesha kuhamia kwenye masoko hayo.
Wakati
huo huo, wakazi wote wa jijini Dar es Salaam katika Manispaa ya
Kinondoni waishio maeneo ya mabondeni wametakiwa kuondoka mara moja
kabla mamlaka haijahukua hatua yoyote ya kubomoa makazi hayo.
Kwa
mujibu wa Mhowera, zoezi hilo linahusisha pia wakazi wote ambao nyumba
zao zimewekwa alama ya X na kupewa hifadhi eneo la Mabwepande nje kidodo
ya Jiji la Dar es Salasaam kutokana na mafuriko yaliyolikumba jiji hilo
Disemba mwaka jana na kuyarudia tena makazi hayo ya zamani.
Aliwataka wakazi hao kuondoka kwenye maeneo hayo na kuhamia katika viuwanja walivyopewa Mabwepande.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment