Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika uwanja wa stendi ya Same
Kuhutubia mkutano wa hadhara leo Oktoba 28, 2012.(PICHA NA IKULU).
Rais
Kikwete ameanzia ziara yake kwenye Wilaya ya Same ambako amehutubia
mkutano wa hadhara kwenye eneo la Stendi ya Mabasi ya mjini Same ambapo
amewaambia mamia ya wananchi kuwa baada ya watu wasioitakia Tanzania
mema kushindwa kuwafarakanisha Watanzania kwa kutumia ukabila sasa
wamegeukia dini.
“Kuna
watu hawana raha na utulivu na amani ya nchi yetu. Walijaribu
kutufarakanisha kwa kutumia ukabila lakini hili lilishindikana na sasa
wamegeukia dini. Lakini ndugu zangu moto wa dini hautakuwa na wa kuuzima
na hautakuwa na mshindi,” Rais Kikwete amewaambia wananchi kwenye
mkutano huo.
Amewataka
Watanzania kuendelea na utulivu wao wa kidini na wakatae kufarakanishwa
kwa tofauti za dini.“Ndugu zangu, siku zote tumekuwa na dini zetu, kila
mmoja akiwa na uhuru wake wa kuabudu anachokitaka na kukiamini na kwa
namna anavyotaka yeye. Ni muhimu tuendelee kuheshimu tofauti zetu za
dini bila kuzigeuza tofauti hizo kuwa chimbuko na sababu ya ugomvi.”
Rais
Kikwete pia amewahakikishia wananchi wa Same kuwa Serikali imedhamiria
kumaliza tatizo la maji katika maeneo ya wilaya hiyo na wilaya za jirani
za Mwanga na Korogwe katika Mkoa wa Tanga.
Amesema
kuwa mradi mkubwa wa kusambaza maji katika vijiji 34 katika wilaya hizo
kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu utaanza kutekelezwa Februari mwakani.
Mradi huo wenye thamani za dola za Marekani bilioni 34 utawahudumia
wananchi katika vijiji 14 vya Wilaya ya Same na utachukua kiasi cha
miezi 18 kukamilika.
“Tutalifanya
suala hili la ukosefu wa maji kuwa historia katika Wilaya ya Same.
Baada ya miezi 18 kuanzia Februari mwakani tutakuwa hatuzungumzi tena
tatizo hilo,” amesisitiza Rais Kikwete huku akishangiliwa sana na
wananchi hao.
Hata
hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa mradi mdogo wa kutoa maji ya dharura
katika Wilaya ya Same utaanza kutekelezwa wiki ijayo wakati pampu za
maji zitakapoletwa kwa ajili ya kufungwa.
Rais
Kikwete ataendelea na ziara yake leo, Jumatatu, Oktoba 29, 2012 kwa
kuzindua Kiwanda cha Tangawizi kilichoko Mamba Miamba na kufanya mkutano
hadhara na wananchi.
Baadaye kesho, Rais Kikwete atazindua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Asha-Rose Migiro iliyoko Mwanga.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Oktoba, 2012
No comments:
Post a Comment