Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima akifungua mkutano
wa wazalishaji wa sukari kutoka nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa
Africa(SADC), unaoendelea jijini Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa wazalishaji wa sukari (TSPA) kutoka nchi za SADC Bw. Aswin Rana akizungumza katika mkutano huo jana.
…………………………………………………..
Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema nchi
inakabiliwa na uhaba wa sukari tani 150,000 kila mwaka kutokana na
uwezo wa viwanda hapa nchini kuzalisha tani 350,00 wakati mahitaji ni
tani 500,000 kwa mwaka.
Hayo yalisemwa na Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alipokuwa akifungua
mkutano wa wazalishaji wa sukari kutoka nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini
mwa Africa(SADC), unaoendelea jijini Dar es Salaam
Malima alisema kiasi hicho ambacho
ni pungufu imekuwa ngumu kukipata kutoka nchi nyingine kwa kuwa nazo
zinahitaji sukari kwa wingi.
“Sisi hatuzalishi sukari kwa
kiwango cha kutosha, tuna mahitaji ya sukari tani laki tano kwa mwaka
sisi tunazalisha tani laki tatu na hamsini hivyo tuna uhaba wa tani laki
moja na nusu ambayo nayo ni ngumu kuipata kutoka kwa wenzetu,”alisema
Malima.
Alisema kutokana na hali hiyo
Serikali inaweka mkakati ya kutaka uzalishwaji wa sukari ufikie tani
milioni moja kwa mwaka ndani ya miaka sita ijayo.
“Kutokana na hilo wadau wa sekta hii ni muhimu wakajipanga ili kuhakikisha lengo hilo linatimia,”alisema na kuongeza;
“Tunaangalia maeneo muhimu ya uzalishaji wa miwa ambayo ndiyo inatumika kutengeneza sukari ili kufanikisha hilo.”
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya
Wazalishaji wa Sukari Tanzania(TSPA), Balozi Fadhili Mbaga alisema kwa
mwaka huu wanategemea kuzalisha sukari kiasi cha tani 320,000 kwa kuwa
msimu ni mzuri.
“Mwaka jana tulizalisha tani
80,000 ambayo ilikuwa ni kidogo ila mwaka huu tunatarajia kuzalisha
kiasi kikubwa ambacho bado kitakuwa hakitoshi kwa matumizi ya hapa
nchini,”alisema Balozi Mbaga.
Alisema hivi sasa nchi za SADC
zinazalisha wastani wa tani milioni tano za sukari kwa mwaka ambayo ni
asilimia 3 ya uzalishwaji wa sukari duniani.
Mkutano huo umehudhuriwa na nchi
ya Angola, Botswana, Lesotho, Malawi, Mauritius, Musumbiji, Namibia,
Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
No comments:
Post a Comment