Serikali ya Tanzania imefanikiwa kuainisha (identify) kiasi
cha hekta 100,000 za ardhi ya wakulima wadogo ambao watasaidiwa
kuongeza uzalishaji wa mpunga ili kuiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi
cha tani milioni moja za mpunga katika mwaka mmoja katika hatua ya
kwanza ya kuleta mageuzi ya kilimo nchini.
Zoezi
hilo ni sehemu ya mipango ya Serikali kuainisha kiasi cha hekta 200,000
za wakulima wadogo ili wasaidiwe kuongeza uzalishaji wa mpunga katika
maeneo mbali mbali nchini, na hasa katika Bonde la Mto Kilombero, chini
ya mipango mbali mbali ya kukuza kilimo kwa haraka, kuongeza uzalishaji
wa mazao mbali mbali na kuwatoa wananchi katika umasikini.
Hayo
yameelezwa jana, Jumanne, Oktoba 2, 2012, na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhesimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokutana na
kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kimataifa
ya Maendeleo la Marekani (USAID), Bwana Rajiv Shah (pichani kulia),
katika Hoteli ya JW Marriott, mjini New York, Marekani ambako Rais
Kikwete amefikia katika ziara yake ya siku mbili.
Rais
Kikwete na Bw. Shah wamejadili mipango mbali mbali inayosaidiwa na
USAID, washirika wengine wa maendeleo na makampuni binafsi ya kimataifa
katika jitihada za Tanzania kukuza kilimo na kupunguza umasikini ukiwamo
ule wa SACGOT, Grow Africa na New Alliance for Agriculture.
Rais
Kikwete amemweleza Shah kuwa mkulima mdogo na ardhi yake, hata ni ndogo
kiasi gani, ni muhimu na ni sehemu maalum ya mipango ya Serikali katika
kuendeleza kilimo kwa kumwinua mkulima huyo mdogo kutoka kwenye
umasikini kwa kumsaidia kuboresha kilimo chake na uzalishaji wake.
“Kwa
hakika, mkulima mdogo ni kiungo muhimu sana katika jitihada zetu. Lazima
tutamsaidia kumtoa kwenye umasikini kwa kuongeza thamani kwenye ardhi
yake, hata kama ni ndogo kiasi gani. Wakipewa pembejeo na misaada
mingine wanaweza kuonyesha maajabu,” amesema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete pia amemweleza Bw. Shah kuhusu mipango ya Serikali ya kuanzisha
Soko la Mazao ambalo litakuwa mkombozi kwa mkulima wa Tanzania na pia
kuunda chombo maalum cha kushughulikia mageuzi katika kilimo cha
Tanzania.
Bw. Shah
amemwahidi Rais Kikwete kuwa Serikali ya Marekani kupitia USAID itakuwa
tayari kusaidia jitihada hizo za Serikali katika kuunda vyombo hivyo
viwili ili kumsaidia mkulima na kilimo cha Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
3 Oktoba, 2012
No comments:
Post a Comment