Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, November 19, 2012

MADIWANI WA CHADEMA ARUSHA WAIBUA GUMZO.



MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na maendeleo(Chadema) wilayani Arusha  waliogoma kumtambua Meya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo sasa wanadaiwa kuanza kumtambua kwa kupitia ‘mlango wa nyuma’.
Tangu ufanyike uchaguzi wa meya wa Jiji la Arusha, kumeibuka mvutano wa kisiasa uliosababisha Chadema wawatangazie wananchi kutomtambua Meya huyo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Omari Mkombole akizungumzia matumizi ya fedha zilizotumika katika uzinduzi wa Jiji hilo hivi karibuni alisema kwamba 
madiwani wa vyama vyote walishiriki vikao muhimu vya kufanikisha sherehe hizo.
 Lakini itakumbukwa ya kwamba msimamo wa madiwani wa Chadema kutomtambua meya huyo ulikuwa ni kutoshiriki vikao vyote vya jiji hilo kama ishara ya kusimamia msimamo wao.
 Tayari baadhi ya makada wa Chadema jijini hapa wametoa msimamo wao kwa nyakati tofauti wakati wakihojiwa kuhusiana na hali hiyo ambapo baadhi ya wamelaani kitendo hicho huku wakienda mbali zaidi na kusema kwamba kitendo hicho ni unafiki mkubwa.
“Taarifa zilizonukuliwa nje kama ni siri zilikuwa ni makisio ya bajeti ambayo baada ya kupitiwa ilibadilishwa na kupata bajeti halisi ya sherehe, hili si siri nyaraka madiwani waliohudhuria wanazo vikao vyote hivi vilifanyika kwa ushirikiano wa madiwani wa Tlp, Chadema wasiokuwa na mivutano na chama chao na CCM chini ya Meya wa Jiji la Arusha,” alisema Mkombole
 Mkombole, akichanganua fedha hizo alisema, zilikuwa ni Sh. 123,689,550 milioni ambapo Mamlaka ya Maji Safi na Taka Arusha (AUWSA) walichangia Sh. 18,156,500 fedha zilizokarabati mnara wa Azimio la Arusha.
 Alisema mdau mwingine Kampuni ya Jiangxi- Geo –Engeneering (Group) Corporation inayojenga barabara za Jiji la Arusha ilichangia Sh, 12 milioni , kampuni ya China Railway Seventh Group Co Ltd  ilichangia Sh , 4 milioni na kufanya jumla ya Sh Milioni 35 kuchangwa na wadau.
 “Halmashauri ya Jiji la Arusha yenyewe imetumia Sh,89,533,050 milioni kugharamia sherehe hizo kwa shughuli mbalimbali zilizobakia mbali na kuwalipa wasanii mbalimbali walioalikwa, fedha hizo pia zilitumika kugharamia chakula cha Rais Kikwete, msafara wake  na wageni waalikwa Hoteli ya Mt. Meru,” alifafanua kaimu mkurugenzi huyo
 Akifafanua kuhusu chakula hicho Mkombole alibainisha kwamba kamati iliyokuwa inasimamia chakula cha Rais Kikwete ilikuwa ikiongozwa na Efatha Nanyaro ambaye ni diwani wa Kata ya Levolosi (Chadema) akishirikiana na Paul Mathysen Diwani wa Moshono kupitia CCM.
 Alisema ushiriki wa viongozi hao ambao ni wawakilishi wa wananchi jijini Arusha ulionyesha kwamba suala hilo lilifanyika kwa ridhaa ya Baraza la Madiwani kwa niaba ya wananchi.
 Alipotafutwa mwenyekiti wa madiwani wa Chadema jijini hapa,Isaya Doita ambaye ni diwani wa kata ya Ngarenaro alikiri wao kushiriki hatua zote katika maandalizi ya uzinduzi wa jiji hilo na kudai kuwa walipokea posho kwa kuwa ni haki yao na wana njia mbalimbali za kutomtambua meya wa jiji la Arusha.

No comments:

Post a Comment