Rais Barack Obama akiwasili Burma.
Rais Barack Obama wa Marekani leo anafanya ziara ya kihistoria nchini Myanmar inayolenga kuhimiza mageuzi ya kisiasa.
Rais Obama atakuwa rais wa kwanza wa Marekani kukanyaga Myanmar huku nchi hiyo ikichipuka kutoka miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi na kutengwa na jamii ya kimataifa.
 Anatarajiwa kumpongeza rais wa taifa hilo Thein Sein, kwa kuimaliza enzi ya utawala wa kijeshi na kumruhusu kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi, kuingia katika ulingo wa siasa.
Rais Obama atakutana pia na Aung San Suu Kyi nyumbani kwake alikotumikia kifungo cha nyumbani kwa miaka kadhaa.
Baadaye leo Obama atakwenda Cambodia kuhudhuria mkutano wa kilele wa mataifa ya Asia Mashariki.
Hata hivyo Obama atamshinikiza rais Sein kuongeza kasi kuelekea demokrasia halisi.