(picha credit: Blogu ya Mhe. Dkt. F. Ndugulile Mbunge wa Kigamboni, CCM)
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litaanza kuziuza nyumba zake zinazojegwa katika eneo la Kibada katikati ya wiki hii.
NHC iemesema nyumba zake 216 zinazojengwa katika maeneo hayo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, hazitauzwa kwa zaidi ya Shilingi milioni 50, ili kumwezesha mwananchi wa kawaida kuzinunu.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mikoa na Utawala wa NHC, Raymond Mndolwa, wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea miradi ya ujenzi wa nyumba za shirika hilo.
“Kigamboni pale Kibada tuna nyumba za aina mbili, yaani zipo za vyumba viwili na nyingine za vyumba vitatu. Kwa kuwa lengo letu siyo kupata faida bali ni kuwasaidia wananchi ili waweze kumiliki nyumba badala ya kuendelea kupanga, nyumba hizo zitakapoanza kuuzwa hazitauzwa kwa zaidi ya Sh milioni 50. Pamoja na kwamba lengo letu ni hilo, bado tunaiomba Serikali iondoe VAT kwa vifaa vya ujenzi ili nyumba ziweze kuuzwa kwa bei ya chini zaidi,” alisema Mndolwa.
Naye, mmiliki wa Kampuni ya Shibat Enterprises Limited, Edwin Shitindi ambayo imepewa tenda ya kujenga nyumba 104 katika eneo hilo la Kigamboni, alisema atahakikisha nyumba hizo zinakamilika ndani ya miezi mitano kuanzia sasa.  Alisema kampuni yake itajitahidi kuzijenga katika ubora unaotakiwa kwa kuwa zitakapoanza kutumika zitatumiwa na Watanzania.
Wadau ambao wana nia ya kumiliki nyumba kwenye eneo hilo wanashauriwa kutembelea tovuti ya NHC (www.nhctz.com) kuanzia Jumatano ya wiki hii ili kupata maelezo zaidi juu ya bei, ulipaji na umiliki wa nyumba hizo.