Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, February 25, 2013

Hii ndio shule ya Mibuyuni: Shule iliyoshika nafasi ya mwisho kidato cha nne kitaifa


 MATOKEO ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yaliyotangazwa mwanzoni mwa juma, yanaendelea kutawala mijadala mbalimbali kila kona.
Sababu kubwa ya mijadala hiyo kutawala yaweza kuwa ni
 takriban kila familia kuguswa kwa njia moja ama nyingine na matokeo hayo.
Katika matokeo hayo karibu shule zote za umma zimefanya vibaya, zile za kata zikiongoza katika kufelisha, huku ile ya  Mibuyuni iliyopo Kilwa mkoani Lindi ikiwa ya mwisho kabisa katika kundi la shule zenye zaidi ya wanafunzi 40.
Mkuu  msaidizi wa shule hiyo Robart Mzumbi, alisema  kuwa matokeo hayo yalitarajiwa kwa kuwa tangu wanafunzi hao walipoandikishwa kidato cha kwanza, hawakuwa wamefaulu.

Alibainisha kuwa, matokeo ya kidato cha pili ya wanafunzi hao walipofanya mtihani wa taifa mwaka 2010, yalikuwa kiashiria kingine kwamba, hata kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wanafunzi hao hawatafanya vizuri.
Pamoja na hayo, Mzumbi anaeleza kwamba kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kuhakikisha wanafundisha watoto hao na mwisho wafanye vyema, matokeo hayo yamewasikitisha kwa kiasi kikubwa.
Alitaja upungufu wa walimu na umaskini wa kipato kwa jamii  inayozunguka shule hiyo kuwa ni moja ya sababu kubwa zilizosababisha matokeo hayo mabaya.
Mwalimu huyo alibainisha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo hujishughulisha zaidi na biashara ndogo ndogo, badala ya kusoma.

Aliweka wazi kuwa, shule hiyo ilikuwa ya mwisho kati ya shule  3,392 zenye watahiniwa 40 na kuendelea, wakati watahiniwa hao wa mwaka 2012 walipochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2009, ambapo walikuwa na alama za chini.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao walichaguliwa kuanza kidato cha kwanza wakati tayari wengi wao walishaanza kufanya biashara ndogondogo, hivyo walikusanywa kutoka huko mitaani na kupelekwa shule.
“Ndugu yangu shule yetu huwa inafanya vizuri kidogo, angalia matokeo ya kidato cha pili mwaka huu Sekondari ya Mibuyuni imekuwa ya 115 kati ya shule 242 za Kanda ya Kusini, wanafunzi wanane wamefaulu kati ya 25 waliofanya mtihani. Lakini kwa matokeo ya kidato cha nne, kwa kweli wanafunzi waliochaguliwa mwaka 2009, hawakuwa na sifa bali waliokotwa tu ili kujaza darasa,”  alisema na kuongeza:
“Hata mtihani wa kidato cha pili  mwaka 2010, walifanya vibaya sana na shule hii ilikuwa ya  pili kutoka mwisho.”
Mzumbi alisema kwamba shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kukosa maabara, upungufu wa walimu wa sayansi, usafiri na umeme wa uhakika.

Pia ina ukosefu wa maji, nyumba za walimu, mabweni kwa ajili ya watoto wa kike, pamoja na shule kujengwa mbali na makazi ya wananchi.
Alieleza kuwa wanafunzi wengi wanaosoma katika shule mbalimbali za Mkoa wa Lindi, hulazimika kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni.
source:mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment