WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu
pamoja na Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni (CCM), wamenusurika
kuchomwa moto na wafuasi wa Chadema usiku wa kuamkia jana.
Tukio
hilo lilitokea usiku wa manane, baada ya wafuasi wa Chadema,
wakiongozwa na Mbunge wa chama hicho Jimbo la Karatu, Mchungaji Israel
Natse, kuvamia nyumba waliyokuwa wamefikia Nagu na Soni, katika Kata ya
Bashnet, Babati Vijijini, mkoani Manyara.
Wafuasi
hao wa Chadema wanawatuhumu Dk. Nagu na Soni kukutana katika nyumba
hiyo kwa nia ya kupanga mipango ya kutoa rushwa ili kufanikisha uchaguzi
mdogo wa udiwani katika Kata hiyo, unaotarajiwa kufanyika leo, ikiwa ni
pamoja na maeneo mbalimbali nchini.
Chanzo cha MTANZANIA Jumapili kilichokuwa eneo la tukio kililidokeza gazeti hili kuwa Dk. Nagu na Soni
walikwenda
kijijini hapo usiku, wakiwa na magari mawili, kila mmoja na lake na
kufika nyumbani kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Petro Baha, kwa kile
kilichodaiwa kuwa ulikuwa ni mpango wa kupita na kugawa fedha kwa
wananchi usiku huo, ambapo pia inadaiwa ndani ya nyumba hiyo alikuwepo
mgombea udiwani wa Kata hiyo, Nicodemus Gwandu (CCM).
Kitendo
cha Nagu pamoja na Soni kuonekana katika nyumba hiyo kiliwashitua
wafuasi wa Chadema, ambao baada ya muda mfupi walivamia nyumba hiyo
wakiwa na Mbunge wao, Natse, madiwani na msafara wa pikipiki na kutishia
kuichoma moto.
Mtoa
habari wetu huyo alisema kuwa, wafuasi hao wa Chadema waliweka kambi
katika nyumba hiyo kuhakikisha Nagu na Soni hawatoki kwenda kwa wananchi
usiku huo.
Chanzo
chetu kilisema kitendo cha kuzingirwa huku wakitishia nyumba kuchomwa
moto kiliwashitua viongozi hao wa CCM na kuamua kupiga simu polisi,
ambao walifika wakiwa sita muda mfupi baadaye kwa ajili ya kuimarisha
ulinzi hadi walipotoka jana asubuhi.
Inaelezwa
kuwa mgombea wa udiwani wa CCM, Nicodemus, ambaye naye alikuwemo ndani
ya nyumba hiyo pamoja na akina Nagu, yeye alifanikiwa kutoroka mapema
kwa kuruka ukuta na kukimbia.
Alipotafutwa
Dk Nagu ili kupata ukweli kuhusu taarifa hizo, simu yake ya kiganjani
iliita bila mafanikio na hata alipotumiwa ujumbe mfupi nao hakujibu.
Kwa upande Soni, alikiri kuzingirwa na wafuasi hao wa Chadema, lakini alikanusha madai ya mkakati wa kutoa rushwa.
“Ni
wanachama wa Chadema wakiongozwa na Mbunge wa Karatu, Mchungaji Natse
na madiwani karibia wa kata sita pamoja na msururu wa pikipiki, sisi
tulikuja kulala, mimi siku zote huwa nalala kijijini, sasa walikuja
wakaanza kupiga yowe, ndipo wananchi wakatoka. Tulikuwa wanne na magari
mawili,” alisema Soni.
Akielezea
sababu za kwenda kulala katika nyumba hiyo, Soni alisema walifikia
hatua hiyo baada ya kuwapo kwa mpango wa Chadema kufanya fujo.
Alisema
dalili hizo zilianza kuonekana mapema baada ya Dk. Nagu kuwekewa mawe
kwenye daraja la Kambesh, kitendo ambacho kilimfanya ashindwe kuondoka
na kwenda kulala alipoandaliwa Soni.
Akifafanua tuhuma kuwa walikwenda kwa ajili ya kutoa rushwa, Soni alisema kama wafuasi hao wana uhakika wathibitishe madai yao.
“Waje
wathibitishe rushwa gani ya kuwapatia watu wanne, maana ndio
waliokuwemo katika nyumba hiyo, hata mgombea wanayedai alikuwepo alikuja
hapo mara baada ya kusikia yowe, wananchi wamesaidia kuwatawanya,”
alisema Soni.
Mbunge
wa Chadema, Natse alikiri kuwepo katika eneo hilo, baada ya kupatiwa
taarifa kwa njia ya simu na wananchi ambao walimweleza juu ya kuwako kwa
mpango wa kutoa rushwa uliokuwa ukiandaliwa na Nagu pamoja na Soni.
“Kilichotokea
saa 7 usiku tulipigiwa simu na wananchi kuwa Waziri Nagu na Soni
walikuwa eneo la Bashnet, ambalo ndiyo ngome yao ya rushwa na walikwenda
kugawa huko, lakini walipoonekana tu yowe lilipigwa na watu
walikusanyika wakitoka na silaha, ikiwemo mapanga na mikuki,” alisema.
Natse
alisema kuwa baada ya taarifa hizo walikwenda eneo la tukio ili
kuepusha madhara zaidi, kutokana na wananchi hao kudhamiria kuchoma moto
nyumba walimokuwamo vigogo hao wa CCM.
“Tulipofika
tuliwatuliza wananchi, lakini waligoma kuondoka, lakini wao (kina Nagu)
walikuwa wameshapiga simu polisi. Askari walipofika eneo la tukio
tuliwataka wawatoe nje wahusika, lakini walitusihi tukubali wawalinde
mpaka asubuhi asitoke mtu, suala ambalo wananchi waliliafiki, huku wao
wenyewe wakiendelea kuwepo eneo la tukio kuhakikisha kuwa hawatoki
kwenda kugawa rushwa mpaka majira ya saa 11 nilipoondoka hapo,” alisema
Natse.
Uchaguzi
huo unaofanyika leo katika kata ya Bashnet, unawashirikisha wagombea
watatu ambao ni Nicodemus Gwandu wa CCM, Alois Gwandu wa NCCR Mageuzi na
Laurent Tara wa CHADEMA, ambaye kabla ya kuhamia chama hicho alikuwa
diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya NCCR Mageuzi
No comments:
Post a Comment