Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
———————————————-
Na Nathan Mtega,Songea
WAZIRI
Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda
anatarajia kufanya ziara ya siku nane mkoani Ruvuma kuanzia tarehe 14
mpaka 21 Julai mwaka huu kwa ajili ya kukagua miradi mbali mbali ya
maendeleo,kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi iliyokamilika katika
wilaya zote tano za mkoa wa Ruvuma na halmashauri za wilaya zote sita.
Akizungumza
na waadishi wa habari mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amesema
kuwa ziara hiyo ambayo ni ya pili kuifanya mkoani Ruvuma ikitanguliwa na
ziara maalumu aliyoifanya kwa ajili ya uzinduzi wa matrekta mwaka jana
katika wilaya ya Songea itaanza kwa kuwasili mjini Songea loe Jumapili
jioni majira ya saa 10:30 jioni ambapo baada ya kupokelewa na kusomewa
taarifa ya maendeleo ya mkoa kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma siku ya
Jumatatu asubuhi atakwenda wilayani Tunduru katika kijiji cha Milonde
ambako atapokea na kukagua ujenzi wa chuo cha ualimu Kiuma na kisha
kuelekea mjini Tunduru ambako atapokea taarifa ya maendeleo ya wilaya.
Na
atahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika katika
uwanja wa michezo na kisha atarejea Ikulu ndogo na Jumanne asubuhi
ataelekea wilayani Namtumbo ambapo baada ya kupokea taarifa ya maendeleo
ya wilaya Ikulu ndogo na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa
hospitali ya wilaya ya Namtumbo na kupokea taarifa na kuzinduwa mradi
wa machinjio ya kisasa wilayani humo pamoja na kupokea taarifa ya umeme
na kisha kuuzindua rasmi umeme atawahutubia wananchi kwenye mkutano wa
hadhara na kuelekea mjini Songea.
Aidha
amesema kuwa Jumatano asubuhi atakwenda wilaya mpya ya Nyasa na kupokea
taarifa ya maendeleo ya wilaya na kusalimia wananchi katika kijiji cha
Lituhi na kuelekea katika kijiji cha Kihagara ambako ataweka jiwe la
msingi kituo cha Afya cha Kihagara na kuondoka kuelekea Liuli ambako
atasalimia wananchi na kuelekea kijiji cha Lundo kwa ajili ya kuona
fursa ya kilimo cha mpunga na kuelekea Mbamba-bay ambako ataweka jiwe
la msingi jengo la karakana ya boti za kisasa na kisha kuhutubia
wananchi kwenye mkutano wa hadhara na kuzindua rasmi wilaya mpya ya
Nyasa.
Na
siku ya Alhamis Waziri Mkuu ataelekea wilayani Mbinga ambapo baada ya
kupokelewa na kusomewa taarifa ya maendeleo ya wilaya ataelekea kijiji
cha Masumuni kwa ajili ya kutembelea na kukagua shamba darasa la kahawa
na kisha kuelekea kijiji cha Lifakara ambako atapokea taarifa na kuweka
jiwe la msingi kwenye mradi wa kufua umeme na kuelekea kituo cha mabasi
ambako atapokea taarifa na kuweka jiwe la msingi kwenye kituo hicho na
kisha atapokea taarifa,kukagua na kuweka jiwe la msingi katika kituo
kidogo cha mradi wa kupeleka umeme Mbamba- bay wilayani Nyasa na kisha
kuwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara .
Mkuu
wa Mkoa amesema kuwa siku ya Ijumaa asubuhi Waziri Mkuu ataelekea
kijiji cha Kitai wilayani Songea na kuelekea kijiji cha Mkenda ambako
atapokea taarifa ya maendeleo ya wilaya na kuweka jiwe la msingi ujenzi
wa soko la kimataifa la Mkenda na kisha ataelekea kijiji cha Mitimbi
ambako atazindua ununuzi wa mahindi msimu wa wa mwaka 2013 katika kanda
ya Songea na kuelekea Ikulu ndogo Songea ambako siku ya Jumamosi ataweka
jiwe la msingi ofisi ya uhamiaji ya mkoa wa Ruvuma na kisha kuelekea
Luhira ambako atatembelea na kupokea taarifa ya uzalishaji wa vifaranga
vya samaki na kisha atapokea taarifa ya maendeleo ya chuo cha ufundi
stadi(VETA) na uzinduzi wa chuo hicho na kisha kuhutubia mkutano wa
hadhara katika viwanja vya Manispaa Songea na Jumapili asubuhi atafanya
majumuisho ya ziara hiyo . na Jumapili asubuhi ataondoka kurejea jijini
Dar Es Salaam.
Habari na picha kwa hisani ya www.demashonews.blogspot.com
No comments:
Post a Comment