DADA
wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Grace
Mbowe, amejiunga na Chama Cha Mapinduzi ( CCM) akitokea Chadema, kwa
kile alichodai haoni jambo jipya katika chama hicho.
Grace amesema amehama kutokana na kuwepo
propaganda zisizotekelezeka. Hata hivyo, amesisitiza kwamba kuwepo kwake
katika Chadema, siyo kwa sababu ya familia.
Alikabidhi kadi hiyo jana kwenye ofisi za
CCM Wilaya ya Hai. Alisema itikadi za kisiasa, zisihusishe masuala ya
kifamilia, kwani upendo wao uko pale pale.
Alisema kilichomfanya kujiunga na chama hicho ni utashi wake. Alidai CHADEMA wanafanya propaganda za kuwadanganya wananchi.Alisema
itikadi za chama, haziwezi kuingilia masuala ya kifamilia, hivyo kwake
siyo ajabu kuondoka CHADEMA, kwani kila mtu ana utashi wake wa kisiasa.
“Nimeamua
kwa hiari yangu mwenyewe bila kushawishiwa na mtu, ndio maana nimetoka
Dar es Salaam kuja Hai kwa ajili ya kurejesha kadi ya CHADEMA na
kujiunga na CCM, suala la itikadi lisihusishe masuala ya kifamilia kwani
upendo wetu upo palepale,”alisema Mbowe.
Alisema, “kuwapo kwangu CHADEMA siyo kwa
sababu ya familia, hivyo hakuna wa kunizuia, natoka kwa utashi wangu, na
tutaendelea kuheshimiana na mdogo wangu Freeman Mbowe katika masuala ya
kifamilia.”
“Freeman Mbowe ni mdogo wangu wa
kuzaliwa kabisa, hakunishawishi kuingia CHADEMA, hivyo sioni haja ya
kuendelea kubaki huku wakati sioni jambo jipya, mimi tangu naifahamu CCM
iko vile vile, bali propaganda za upinzani ndizo zinawalaghai
wananchi,” alisema.
Aliviasa
vyama vya siasa, kuwa sasa umefika wakati wa kuacha malumbano na
maandamano ya itikadi, yasiyokuwa na faida yoyote, badala yake huu ni
muda wa kujenga nchi kwa ushirikiano.
Awali, akipokea kadi ya CHADEMA, Katibu wa
CCM Wilaya ya Hai, Hassan Mtenga alisema alichokifanya Grace ni uamuzi
wa busara, baada ya kutazama Chadema ilipo na inapokwenda.
Alisema wimbi la wanachama wa Chadema
kurudisha kadi na kujiunga na CCM, limekuwa kubwa wilayani Hai. Alisema
tangu Januari hadi sasa amepokea wanachama 530.
Mtenga aliwataka wananchi kutambua
kwamba Jimbo la Hai, siyo kitovu cha upinzani bali CHADEMA ni chama
kilichotoa upinzani kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa 2010. Alisema hali
hiyo, ilitokana na makundi ya CCM.
Alisema kwa sasa watu asitarajie tena suala hilo kutokea. --- via HabariLeo
No comments:
Post a Comment