MAHAKAMA ya
Wilaya ya Kinondoni imetupilia mbali pingamizi la mke wa aliyekuwa
Mkurugenzi wa Utumishi wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, Aurelia Ngowi
la kupinga mumewe kuuza mali za familia na kumfukuza kwenye nyumba
wanayoishi.
Kesi hiyo
imefunguliwa mbele ya Hakimu Jackline Rugemalila katika mahakama hiyo,
Dar es Salaam. Mahakama hiyo ilihamia Mbezi Africana iliko nyumba hiyo
kufanya ukaguzi ili kujiridhisha juu ya pingamizi zilizotolewa na pande
zote mbili.
Ngowi alipinga mumewe kuuza
mali za familia na kumfukuza, wakati kesi ya msingi ya madai ya talaka
ikiendelea, jambo ambalo Liyumba akiongozwa na Wakili wake Sweetbert
Nkuba alikuwa akilipinga, kwa kudai nyumba hiyo ni ya biashara na si ya
kuishi familia, kama inavyodaiwa.
“Baada ya kusikiliza pande
zote mbili, mahakama hii imeona kuwa nyumba hiyo ni ya biashara na si ya
kuishi familia, kama ilivyoelezwa katika zuio la mshitaki,” alisema
Hakimu Rugemalila.
Katika hati ya madai, Aurelia
anaiomba mahakama iweke zuio la muda ili Liyumba asiuze mali za familia,
pia asiuze nyumba iliyopo Africana Mbezi Beach katika kiwanja namba
2232/2233, ambayo walikuwa wanaitumia kama makazi ya familia.
Anaiomba mahakama iamuru
waendelee kuishi katika nyumba hiyo, wakati shauri hilo la likiendelea,
pia alipe gharama za uendeshaji wa kesi.
Katika hati ya kiapo,
inayounga mkono madai yake, Aurelia anadai alifunga ndoa na Liyumba
mwaka 1978 mkoani Kilimanjaro na kupata watoto wanne.
Anadai mwaka 1980 walianza
kuishi kwenye nyumba iliyopo Africana. Anadai waliendelea kuishi katika
nyumba hiyo na baadaye waliamua upande wa nyumba, waweke hoteli
inayoitwa Amjen Executive pamoja na biashara nyingine, zilizokuwa
zinawaingizia kipato kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya familia.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo,
baada ya Liyumba kutoka gerezani ambako alikuwa anatumikia kifungo,
alihama nyumbani na kuanza kuuza mali mbalimbali yakiwemo magari,
kiwanja cha ekari 50 kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani na kiwanja cha
Tabata.
Alidai kuwa Julai 18 mwaka
huu, Liyumba aliwafukuza yeye na watoto wake na kufunga nyumba hiyo
pamoja na eneo la biashara, waliyokuwa wakiitegemea kwa ajili ya kupata
fedha za matumizi ya kila siku, kisha akaweka walinzi ambao wanawazuia
kuingia.
Aurelia alidai baada ya
kufanya uchunguzi, aligundua kuwa mume wake anauza mali walizochuma
pamoja. Alidai endapo mahakama haitaweka zuio, atapata hasara kubwa.
Liyumba alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kupatikana
na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma.
Alimaliza kutumikia kifungo
hicho Septemba 23 mwaka juzi. Kesi ya msingi ya madai ya talaka,
itatajwa tena Septemba 16, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment