Abdallah Khamis, Mlele
NAIBU
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe,
amesema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni mzigo katika serikali.(hd)
Amesema
kuwa hii ni kutokana na kushindwa kufanya uamuzi mgumu katika masuala
yanayolihusu taifa licha ya baadhi ya mambo kuwa katika mamlaka yake.
Zitto
alisema kuwa hivi karibuni Pinda alishindwa kusimamia muswada wa sheria
ya marekebisho ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, hali
iliyosababisha kutokea vurugu bungeni.
Zitto
ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alitoa kauli hiyo juzi wakati
akihutubia mikutano ya hadhara katika kata ya Inyonga na Songambele
wilayani Mlele, mkoa wa Katavi, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya
kuimarisha chama Kanda ya Magharibi.
Alisema
ni jambo la kusikitisha kuona Waziri Mkuu akishindwa kukutana na
kiongozi wa upinzani bungeni na kujadili masuala muhimu ya kitaifa kabla
ya Bunge kuanza kwa ajili ya mustakabali wa taifa.
Akitolea
mfano masuala kadhaa ambayo Pinda ameshindwa kuyasimamia na kumsubiri
Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuyafanyia uamuzi, Zitto alitaja sakata la
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, na
Yule wa Wizara ya Afya na sasa suala la kuhakikisha muafaka unapatikana
katika suala muhimu la Kikatiba.
"Kama
tunaye Waziri Mkuu anayekaa bungeni na kushika tama wakati nchi ikiwa
katika hali ngumu ni tatizo. Huyu kila jambo anasubiri Rais atoke UN
kuja kufanya uamuzi ambao yeye angeweza kuusimamia. Basi tuna kazi ya
ziada katika kupata maendeleo," alisema.
Zitto
alifafanua kuwa mwanzoni alidhani Pinda anashindwa kusimamia majukumu ya
serikali kutokana na kukabiliwa na jitihada za kuboresha miundombinu na
maisha ya wakazi wa jimbo lake hali aliyoelezea kuwa ni tofauti na
aliyoikuta.
Alisema
kutokana na hali hiyo ya Pinda kutokuwa na mamlaka, wakulima wa Katavi
wameendelea kununua mbolea kwa gharama ya juu licha ya serikali kutenga
kiasi cha bilioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya ruzuku ya mbolea kote
nchini.
Alisema fedha hizo zinaliwa na wajanja huku serikali ikiendelea kuwa katika hali ya usingizi wa pono.
Tofauti ya CCM, CHADEMA
Akizungumzia
sababu ya ziara yake katika kanda hiyo, Zitto alisema ni kwa ajili ya
kuhimiza mbegu ya ukombozi wa fikra na maendeleo kutoka katika mikono ya
Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alisema
wakati CHADEMA inapambana katika kila kona kuhakikisha udhalimu
unaofanywa na serikali unaondoka, CCM inatumia kila njia kuhakikisha
inawanyonya wananchi.
"Tofauti
kubwa kati ya vyama hivi ni kwamba CCM inaishi kwa kuwanyonya wananchi
na CHADEMA imesimama kidete kutaka udhalimu huo uondoke; na kwa ajili
hiyo chama hicho tawala kinatumia kila propaganda kuhakikisha wananchi
hawatuungi mkono," alisema.
Kwa
mujibu wa Zitto, kazi ya CHADEMA siku zote imekuwa ni kuwafumbua macho
wananchi juu ya unyonyaji unaofanywa na serikali ya CCM na kuwataka
waepukane na propaganda za kwamba kuiunga mkono CHADEMA ni kukaribisha
vita nchini.
Alisisitiza
kuwa kwa sasa CHADEMA inajiandaa kushika dola mwaka 2015 na kwamba
wanasimamia upatikanaji wa Katiba bora itakayowafanya wanasiasa kuwa
watumishi wa wananachi badala ya kuwa watawala.
"Mmetuona
kwa uchache wetu bungeni tumeweza kufanya mambo makubwa kwa nchi kila
kashfa ya ufisadi mnayoisikia leo ni wabunge wa upinzani wameibua na si
wa chama tawala," alisema.
No comments:
Post a Comment