Shehe Semtawa
HUDUMA za
usafiri katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi
cha Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam, jana zilisimama kwa muda kutokana
na madereva wa malori kufunga barabara katika kituo cha mizani cha
Kibaha tangu juzi usiku.
Hali hiyo
ilileta usumbufu mkubwa kwa abiria waliokuwa wasafiri kwenda nje ya
jiji, kwani mabasi yalikosa mahali pa kupita na hivyo kulazimika
kusitisha safari.
Msongamano
huo ulisababishwa na hatua ya madereva wa malori yanayobeba mizigo
yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea, kuamua kuegesha magari yao
barabarani kupinga kitendo cha serikali kufuta msamaha wa tozo ya
asilimia tano ya mizani.
Akikizungumza
kwa niaba ya madereva wenzake wa mabasi, Salimu Kangeta alisema hawako
tayari kuwatoa abiria kituoni huku wakijua kuwa watakwenda kuteseka huko
mbele.
Kangeta
alifafanua kuwa abiria walifika asubuhi kama tiketi zao zilivyokuwa
zikiwaelekeza lakini baadhi yao walishindwa kuondoka kutokana na
madereva wengi kukataa kuanza safari kwa sababu barabara ilikuwa na
msongamano mkubwa wa malori kuanzia Kibamba hadi Kibaha mizani.
Alisema
kuwa katika kuhangaika, wako madereva waliojaribu kupitia njia ya
Bagamoyo lakini ilishindikana baada ya kuzuiwa na askari kwa madai kuwa
kisheria hawaruhusiwi kupita katika barabara hiyo.
"Kuna
askari ambaye hatukumfahamu alikuwa akielekeza madereva kupitia njia
hiyo kwa madai alikuwa amewasiliana na RTO wa mkoa wa Pwani kuhusu
mpango huo.
"Cha
kushangaza baadhi ya madereva walizuiwa kupita katika njia hiyo ya
Bagamoyo na kutakiwa kurudi barabara ya Morogoro, huu ni usumbufu tu,"
alisema.
Kwa
mujibu wa dereva huyo, hata kama wangeruhusiwa kupita huko bado magari
yanayopita mkoa wa Morogoro kwenda mikoa mingine yasingenufaika na
utaratibu huo, bali yale ya kwenda mikoa ya kaskazini pekee.
Kangeta
alisema madereva hawapaswi kulaumiwa kwa usumbufu walioupata abiria
kwani wao sio chanzo bali wa kulaumiwa ni Wakala wa Barabara Nchini
(Tanroads) na kikosi cha usalama barabarani kwa kushindwa kudhibiti
tukio hilo mapema.
Uegeshaji
huo wa malori na kufunga barabara ulianza juzi saa 10 jioni kwenye
mizani ya Kibaha baada ya wamiliki wa malori kuwa na mkutano wa kupinga
tozo ya asilimia tano ya mizani, ambayo ilikuwa imefutwa.
Aidha
katika mkutano huo ilielezwa na wamiliki hao kuwa hali hiyo itasababisha
kero kubwa sio kwa wenye malori pekee, bali hata kwenye mizani pia.
Msemaji
wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema suala la msongamano huo ni la
kiutawala, hivyo wenye kulitolea ufafanunuzi zaidi ni kikosi cha
usalaama barabarani.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili baadaye mchana zilisema kuwa mabasi mengi
yalianza safari zao mchana saa sita baada kukwama kuondoka asubuhi.
No comments:
Post a Comment