Na Mahmoud Zubeiry
TIMU ya soka
ya taifa ya wanawake kwa vijana chini ya umri wa miaka 20, The
Tanzanites imeifunga Msumbiji mabao 10-0 katika mechi ya kwanza ya
raundi ya Kwanza ya Kombe la Dunia kwa mabinti wa umri huo, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
Katika mchezo huo uliohudhuria na mashabiki wachache mno, hadi mapumziko, tayari Tanzanites walikuwa mbele kwa mabao 5-0.
Bao la kwanza
lilifungwa dakika ya sita na Neema Paul aliyeunganisha pasi ya Theresa
Yona, kutoka wingi ya kushoto, wakati mfungaji bora wa michuano ya
kimataifa ya Airtel Rising Stars iliyofanyika mwaka huu Nigeria, Shelder
Boniface alifunga la pili dakika ya 24 baada ya kupangua ngome na
kumpiga chenga hadi kipa.
Deonesia Daniel akafunga bao la tatu kwa shuti kali la mpira wa
adhabu lililotinga moja kwa moja nyavuni dakika ya 32 na dakika ya 41,
Amina Ali akafunga la nne kwa shuti kali kutoka nje ya eneo la mita 18.
Shelider Boniface alifunga bao ambalo lingekuwa la tano dakika ya 45, lakini refa Ines Niyonsara wa Burundi akakataa.
Kipindi cha pili The Tanzanites inayofundishwa na Rogasian Kaijage
ilirudi na moto wake na kufanikiwa kupata bao tano, mfungaji Neema Paul
aliyeunganisha krosi ya Theresa Yona.
Hatimaye Shelder alifunga bao la sita dakika ya 80 akimalizia mpira uliotemwa na kipa kufuatia shuti la Stumai Abdallah.
Dakika ya 82 Tanzania ikapata bao saba kupitia kwa Amina Ali aliyefumua shuti kutoka katikati ya Uwanja.
Tanzanites
walipata bao la nane dakika ya 86 kupitia kwa Deonesia Daniel aliyefunga
kwa mkwaju wa penalti, baada ya Shelder Boniface kuangushwa kwenye eneo
la hatari.
Dakika ya 89 Tanzania ilipata bao tisa kupitia kwa Amina Ali tena,
ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo. Stumai Abdallah akaifungia Tanzania
bao la 10 dakika ya 90.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Celina Julius, Stumai Abdallah, Maimuna
Said/Amina Hebron dk60, Fatuma Issa, Anastazia Anthony, Deonisia
Daniel, Vumilia Maarifa, Amina Ali, Neema Paul, Shlder Boniface na
Theresa Yona.
Msumbiji; Paulina Jambo/Catarina Francue dk50, Esperanca
Malaita/Delice Assane dk52, Felismisa Moiane, Emma Paulino, Gilda
Macamo, Deolinda Gove, Jessica Zunguene, Cidalia Cuta, Nelia Magate,
LonicaTsanwane na Onesema David.


No comments:
Post a Comment