Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, October 26, 2013

Wapiganaji 40 wa upinzani wauwawa Syria


016899688_30300_0c893.jpg
Wanajeshi wa serikali ya Syria jana wamewavamia waasi karibu na mji mkuu, Damascus, na kuwaua wapiganaji wapatao 40 wa upinzani. Mji wa kaskazini wa Safira, kusini mashariki mwa Aleppo, pia umeshambuliwa.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari uvamizi huo ulikuwa sehemu ya operesheni ya jeshi dhidi ya ngome za waasi zinazouzunguka mji huo, makao makuu ya utawala wa rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad. Uvamizi huo karibu na Damascus umefanywa saa chache baada ya vikosi vya rais Assad kuuteka mji wa Hatitat al-Turkomen, kusini mwa mji huo, na hivyo kudhibiti barabara muhimu inayouunganisha mji huo mkuu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Damascus.
Shirika la habari la serikali, SANA, limesema waasi 40 wameuwawa katika hujuma hiyo iliyotokea karibu na eneo la Otaiba, na kwamba shehena kubwa ya silaha imepatikana, yakiwemo makombora ya kuripua vifaru. Eneo hilo ni sehemu ya ukanda unaojulikana kama Ghouta Masharki, ambako kulifanyika shambulizi la silaha za sumu mwezi Agosti mwaka huu, ambapo mamia ya watu waliuwawa, wakiwemo wanawake na watoto.
Afisa mmoja wa jeshi ambaye jina lake halikutajwa, ameiambia televisheni ya taifa ya Al-Ikhbariya kwamba wapiganaji wa kigeni ni miongoni mwa waliouwawa na shambulizi hilo limefanywa baada ya kupata taarifa za kijasusi. "Ilikuwa operesheni iliyofanikiwa. Tutaendelea kupata ushindi kutoka sehemu moja hadi nyengine," akaongeza kusema afisa huyo.
Mwanajeshi mwingine, ambaye hakutambulishwa kwa majina, amesema waasi ni wa kundi la Islam Brigade na Jabhat al Nusra au Al Nusra Front, lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda. Shirika la haki za binaadamu la Syria lenye makao yake jijini London, Uingereza limesema wapiganaji wapatao 20 wameuwawa katika uvamizi huo, lakini halikutoa maelezo zaidi.
Wakati huo huo, helikopta za jeshi zimeushambulia mji wa kaskazini wa Safira, kusini mashariki mwa Aleppo. Kambi kubwa ya jeshi karibu na mji huo inaaminiwa ina kituo cha chini ya ardhi cha kinachotumiwa kutengeneza na kuhifadhi silaha za sumu. Shirika la madaktari wasio na mipaka limesema watu 130,000 wameukimbia mji wa Safria mwezi huu na kwamba mji huo umekuwa ukishambuliwa kwa mabomu tangu Oktoba 8. Taarifa ya shirika hilo imesema watu 76 wamekufa mjini humo.
Shambulizi la bomu
Katika tukio lengine la machafuko, shirika hilo limeripoti kuwa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya motokaa limelipuka nje ya msikiti katika kijiji cha Suq Wadi Barada, na watu 40 ama wameuwawa au kujeruhiwa katika mlipuko huo. Hakuna taarifa za idadi kamili ya watu waliouwawa au kujeruhiwa katika mji huo, unaopatikana kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Damascus.
Mkurugenzi wa shirika la haki za binaadamu la Syria, Rami Abdel Rahman, amesema miongoni mwa waliojeruhiwa ni watoto. Rahman aidha amesema ingawa mji huo uko mikononi mwa waasi, wanajeshi wanaomtii rais Assad wameuzingira. Televisheni ya taifa imeripoti juu ya shambulizi hilo, ikiwashutumu magaidi wenye mafungamano na al Qaeda. "Waasi wa kundi la Al Nusra Front wamelipua bomu karibu na msikiti wa Osama Bin Zeid katika kijiji cha Suq Wadi Barada katika mkoa wa Damascus. Taarifa za awali zinasema watu wameuwawa na wengine kujeruhiwa," ikatangaza televisheni hiyo.
Mapambano ya Wakurdi
Kuhusu mapambano kati ya Wakurdi na wapiganaji wa jihad shirika hilo limesema wapiganaji wa kikurdi wamezidi kusonga mbele katika mkoa wa Hassaekh wenye idadi kubwa ya Wakurdi. Wapiganaji hao waliingia mji wa Yaaroubiyeh leo na kukabiliana na makundi kadhaa ya jihad, yakiwemo Islamic State of Iraq na Al Nusra Front, yenye mafungamano na kundi la al Qaeda.
Mji wa Yaaroubiyeh unaodhibitiwa na waasi uko katika kivuko kikuu cha mapakani kuingia nchini Iraq na kuuteka mji huo kutawapa wapiganaji wa Kikurdi njia rahisi ya kusafirishia bidhaa na mahitaji mengine kutoka eneo la Wakurid kaskazini mwa Iraq. Eneo hilo limeshuhudia mapiganao makali katika siku za nyuma na mapambano makali kati ya wapigaji wa Kikurdi na wapiganaji wa makundi ya jihad kaskazini mwa Syria yamesababisha vifo vya mamia ya watu katika miezi iliyopita.
Pia mwezi Machi mwaka huu wanaume waliokuwa wamejihami na bunduki waliwaua wanajeshi 51 wa Syria baada ya kuvuka na kuingia Iray kutoka Yaaroubiyeh. Wanajeshi hao walikuwa wameingia Iraq kutafuta hifadhi kufuatia mapambano na waasi upande wa Syria wa mpaka.
Mwandishi. Josephat Charo/APE/AFPE

No comments:

Post a Comment